Shamkhani: Mashinikizo ya juu yamefelishwa na sera ya muqawama
-
Ali Shamkhani
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema stratejia ya muqawama amilifu ndiyo iliyoishinda na kusambaratisha sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Iran.
Ali Shamkhani alisema hayo jana kwenye ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kueleza kuwa, viongozi wa serikali ya sasa ya Marekani wamesikika mara kadhaa wakiungama kwamba, sera ya mashinikizo ya juu kabisa ya nchi hiyo dhidi ya Iran imefeli.
Amesema mashinikizo ya juu kabisa ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamefeli kutokana na kusimama kidete Iran na kufungamana kwake na sera ya mapambano ya kiwango cha juu kabisa.
Shamkhani amesisitiza kuwa: Iwapo mazungumzo ya Vienna hayatapelekea kufikiwa makubaliano mazuri, utawala wa sasa wa Marekani utashindwa vibaya katika mustakabali wa karibu, kwa kushindwa kutumia fursa zilizojitokeza za kidiplomasia.

Katika kutekeleza sera iliyopewa jina la mashinikizo ya juu kabisa, baada ya aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump kuchukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei, 2018, Washington ilirejesha tena vikwazo vilivyositishwa dhidi ya Iran kupitia makubaliano hayo na hata akapitisha vikwazo vingine vipya pia; lakini sera hiyo imeshindwa na kugonga mwamba kikamilifu.
Mashinikizo hayo ya Marekani hadi sasa yameshindwa kufikia malengo yaliyokuwa yamekusudiwa na utawala wa Trump. Kadhalika utawala wa sasa Rais Joe Biden haujachukua hatua za maana za kuiondolea Iran mashinikizo hayo yaliyowekwa na mtangulizi wake.