Eslami: IAEA isichukue misimamo ya kisiasa kuhusu Iran
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesisitiza kuwa, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unapaswa kuchukua msimamo usio wa kisiasa kuhusu Iran.
Mohammad Eslami ameyasema hayo leo mjini Tehran katika mkutano wa pamoja na waandishi habari na Rafael Mariano Grossi Mkurugenzi Mkuu wa IAEA na kuongeza kuwa: "Ni matumaini kuwa uharibifu ambao umefanywa na maadui dhidi ya Iran na mfano mdogo ni kuuawa wataalamu wa nyuklia wa Iran, utakomeshwa."
Eslami ameongeza kuwa, Iran ina mpango wa muda mrefu wa kustawisha mpango wake wa nyuklia kwa malengo ya amani.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, amesema uwezo wa kisheria wa IAEA unapaswa kutumiwa kuunga mkono shughuli za nyuklia za Iran kwa malengo ya amani.
Eslami ameendelea kusema kuwa, masuala ya nyuklia yanapaswa kutatuliwa kwa njia ya kawaida bila kuingizwa siasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa IAEA amesema amekuwa na mazungumzo mazuri na Eslami. Amesema kuna umuhumu mkubwa wa kuhakikisha kuwa pande mbili zinafahamiana ili kuwepo na ushirikiano na kwamba nishati ya nyuklia ni muhimu kwa maendeleo ya nchi zote ikiwemo Iran. Aidha amelalamika kuwa, baadhi ya wanachama wa IAEA hawalindi ripoti za siri za wakala huo kuhusu Iran.
Akiwa mjini Tehran Grossi pia amefanya mazungumzo na Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.