Amir Abdollahian: Iran inaunga mkono juhudi za kutatua mzozo wa Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono juhudi za kisiasa za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Ukraine.
Wakizungumza kwa njia ya simu, Hossein Amir-Abdollahian na mwenzake wa Ukraine, Dmitry Kolba wamejadili mzozo wa Ukraine na kutilia mkazo udharura wa kulindwa vituo vya kidiplomasia, kutumwa kwa misaada ya kibinadamu na masuala yanayozihusu nchi mbili.
Amir Abdollahian sambamba na kuelezea msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kupinga vita na haja ya kuzingatia utatuzi wa kisiasa na mazungumzo ya kidiplomasia, amekitaja kikao cha hivi karibuni cha mawaziri wa mambo ya nje wa Ukraine na Russia nchini Uturuki kuwa muhimu na kusisitiza udharura wa kuendelea na kuimarisha njia ya kisiasa ya kutafuta ufumbuzi wa mzozo wa Ukraine.
Akizungumzia chimbuko na chanzo cha mgogoro wa Ukraine, Amir Abdollahian amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono juhudi zote za kisiasa za kutatua mgogoro huu." Ameongeza kuwa Tehran haina sera za kiundumakuwili na inapinga vita vya aina zote vikiwemo vya Ukraine, Yemen, Afghanistan na kwengineko.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu imetuma misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Ukraine walioko kwenye mpaka wa nchi hiyo na Poland na kwamba inakusudia kutuma timu ya madaktari kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa wakimbizi hao.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine ameishukuru Iran kutokana na msimamo wake wa kupinga vita na kutuma misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi walioko kwenye mpaka wa Ukraine na Poland na kusisitiza kuwa serikali ya Kyiv inafanya kila iwezalo kulinda vituo vya kidiplomasia vikiwemo vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.