Mpira wa mazungumzo ya Vienna kwenye uwanja wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82132-mpira_wa_mazungumzo_ya_vienna_kwenye_uwanja_wa_marekani
Katika mazungumzo yake ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuondolewa vikwazo huko Vienna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Jamhuri ya Kiislamu imewasilisha mapendekezo yake kwa Marekani kuhusu masuala yaliyosalia kupitia mpatanishi mkuu wa Umoja wa Ulaya."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2022 06:31 UTC
  • Mpira wa mazungumzo ya Vienna kwenye uwanja wa Marekani

Katika mazungumzo yake ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuondolewa vikwazo huko Vienna, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Jamhuri ya Kiislamu imewasilisha mapendekezo yake kwa Marekani kuhusu masuala yaliyosalia kupitia mpatanishi mkuu wa Umoja wa Ulaya."

Hossein Amir-Abdollahian amemwambia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, kwamba "Tuko karibu kufikia makubaliano katika mazungumzo na tumetoa mapendekezo yetu, na sasa mpira uko katika uwanja wa Marekani."

Duru ya 8 ya mazungumzo ya kuiondolea Iran vikwazo, ambayo ilianza Disemba 27, 2021, iliingia katika hatua muhimu mnamo Machi 11, 2022, kwa pendekezo lililotolewa na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya (EU), Joseph Borrell, na timu zinazoshiriki mazungumzo zimerudi kwenye miji yao mikuu kwa mashauriano ya kisiasa.

Joseph Borrell

Suala la dhamana na kuondolewa majina ya watu  katika orodha nyekundu na ya vikwazo ya Marekani bado ni miongoni mwa mambo ambayo Merekani, kama mkiukaji wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA, haijayachukulia maamuzi muhimu wa kisiasa ya kuyatatua.

Tangu mwanzoni mwa duru ya 8 ya mazungumzo haya, timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayoongozwa na Ali Bagheri Kani, imewasilisha mipango na ubunifu muhimu kwa ajili ya kufikiwa makubaliano; Umoja wa Ulaya na mratibu wa Umoja wa Ulaya. Katika mazungumzo yake ya tarehe 27 Machi na Enrique Mora, Naibu Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na mratibu wa mazungumzo ya Vienna, Ali Bagheri alisisitiza kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa iwapo upande wa Marekani utakuwa na ukweli. Mkabala wake, tarehe 30 Machi Wizara ya Fedha ya Marekani iliwawekea vikwazo vipya baadhi ya watu binafsi na mashirika ya Iran badala ya kuonyesha nia njema katika mazungumzo hayo kwa kuondoa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Sambamba na hatua hiyo, Naibu Waziri wa Fedha wa Marekani, Brian Nelson alisema Washington haitasita kuwalenga wale wanaounga mkono mpango wa kutengeneza makombora ya balistiki wa Iran, hata katika kipindi cha sasa cha kufufua mapatano ya nyuklia ya JCPOA na Iran.

Hata hivyo, msingi wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kuondolewa kikamilifu vikwazo vya kiuchumi, mkabala wa Iran kutekeleza majukumu yake ya kinyuklia, na kimsingi suala hili halina uhusiano wowote na masuala ya ulinzi na sera za kikanda za Jamhuri ya Kiislamu. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi alisisitiza tarehe 20 Machi kwamba: "Hatutafanya muamala wa aina yoyote kuhusu maslahi na usalama wa wananchi. Watu wote wameona kwamba suala la kuzidisha uwezo wa kiulinzi wa nchi, makombora na anga ni jambo linalowekwa mbele, kwa sababu usalama wa nchi ni kipaumbele."

Sayyid Ebrahim Raisi

Ni wazi kuwa suala la kufikia mwafaka katika mazungumzo ya Vienna linailazimu Marekani kuachana na sera zake za kibabe na kupenda makuu, na pia kuchukua hatua madhubuti na za kuaminika.

Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, dhamana ya kufikiwa makubaliano ya kudumu ni kuondolewa kikamilifu vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran na kulindwa maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu katika makubaliano tarajiwa. Hivyo, Iran imetoa mapendekezo na mipango muhimu ya kuhitimisha mazungumzo hayo kwa kuzingatia ukweli huo; na kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alivyosema: "Sasa mpira uko kwenye uwanja wa Marekani." 

Amir Abdollahian

Maafisa wa Washington wanatakiwa kuonesha azma ya kisiasa ya kufikia makubaliano kwa kuwa wakweli na kutoa dhamana ya kuaminika, sambamba na kuacha kutoa madai mapya na ya uongo ambayo hayana uhusiano wowote na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.