Raisi: Uhusiano wa Iran na Kuwait unarejea katika hali yake ya kawaida
Rais wa Iran ameutaja msimamo imara wa Kuwait mkabala wa njama mbalimbali katika eneo la Magharibi mwa Asia kuwa makini; na huku akikumbushia uhusiano mzuri kati ya Iran na Kuwait huko nyuma, amesisitiza kuwa, uhusiano wa pande hizo mbili zikiwa nchi mbili marafiki wa muda mrefu, unapasa kurejea katika uwezo wake halisi.
Dakta Sayyid Ebrahim Raisi jana alasiri alifanya mazungumzo ya simu na Amir wa Kuwait, Sheikh Ahmad Al-Jaber Al-Sabah na akatoa mkono wa kheri na fanaka kwa wananchi wa Kuwait kwa kusherehekea Sikukuu ya Idul-Fitr na kueleza kuwa, anataraji kwamba kwa baraka za Sikukuu hii ya Iddl Fitr, Mwenyezi Mungu atayabariki mataifa jirani na rafiki ya Kuwait na Waislamu wote kwa ujumla.
Raisi ameongeza kuwa: Kukurubiana kwa nyoyo za Waislamu katika minasaba kama hii kunazidisha mshikamano kati ya nchi za Kiislamu.
Rais wa Iran ameeleza matarajio yake ya kukutana na Amir wa Kuwait hapa Tehran na kuongeza kuwa, kuongezeka ziara na mazungumzo kati ya viongozi wa nchi mbili kunaweza kupandisha zaidi kivitendo kiwango cha ushirikiano wa nchi mbili.
Katika mazungumzo hayo ya simu, Sheikh Ahmad Al-Jaber Al-Sabah Amir wa Kuwait amempongeza Rais Ebrahim Raisi na wananchi wa Iran kwa kuwadia Sikukuu ya Idul Fitr na akaeleza kufurahishwa sana na hatua mpya na umuhimu unaonyeshwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Rais Raisi katika kukuza uhusiano na nchi jirani na rafiki.