Dafina za Imam Khomeini kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i8416-dafina_za_imam_khomeini_kwa_mtazamo_wa_kiongozi_muadhamu
Leo Ijumaa, taifa zima la Iran na wapenzi na wafuasi wa njia na fikra za Imam Khomeini MA wameshiriki kwa namna moja au nyinginekatika kumbukumbu za mwaka wa 27 wa kuomboleza siku alipofariki duniani mwanachuoni na shakhsia huyo mkubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 04, 2016 00:04 UTC
  • Dafina za Imam Khomeini kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu

Leo Ijumaa, taifa zima la Iran na wapenzi na wafuasi wa njia na fikra za Imam Khomeini MA wameshiriki kwa namna moja au nyinginekatika kumbukumbu za mwaka wa 27 wa kuomboleza siku alipofariki duniani mwanachuoni na shakhsia huyo mkubwa.

Kwa hapa nchini Iran, umati mkubwa wa waombolezaji umekusanyika katika haram ya mwanachuoni huyo iliyoko kusini mwa Tehran kwa ajili ya maadhimisho hayo ambapo Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa hotuba muhimu na sambamba na kubainisha fikra za kisiasa za Imam Khomeini MA, ametaja sifa za kipekee, vielelezo na fikra za kisiasa za wanachuoni huyo. Amesema, kuwa muumini wa kweli, mcha Mungu na mwanamapinduzi, ni sifa tatu kuu alizokuwa nazo Imam Khomeini MA. Amesema, kwa hakika Imam Khomeini MA alikuwa Imam wa Mapinduzi na neno Mapinduzi ndani yake limesheheni mambo muhimu sana, na Imam Khomeini alikuwa mstari wa mbele katika mambo yote hayo na ndio maana Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakapata ustahiki wa kuitwa Mapinduzi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, sababu kuu inayoyafanya madola ya kiistikbari yayaogope na kuwa na woga kiasi chote hiki kuhusiana na Mapinduzi ya Kiislamu na Imam Khomeini MA ni sifa hizo alizojipamba nazo Imam. Aidha amebainisha kuwa, madola ya kibeberu yanaogopeshwa na sifa za kuwa mwanamapinduzi na kutenda kiuanamapinduzi alizokuwa nazo Imam Khomeini MA. Amesema hatua zilizochukuliwa na mabeberu kama vile mashinikizo ya kiuchumi, vikwazo, njama za kila nui na madai nya kila namna yasiyo na msingi kuhusu masuala kama kadhia ya nyuklia na haki za binadamu, yote hayo ni visingizio tu vya kuficha woga wa mabeberu hao. Amesisitiza kuwa, hivi sasa pia maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wana woga mkubwa kuhusiana na kuendelea taifa la Iran kufanya mambo yake kimapinduzi na kijihadi. Hatua ya Imam Khomeini ya kushikamana na fikra ya kimapinduzi na kutenda mambo kimapinduzi iliandaa uwanja wa kutokea mabadiliko makubwa ya kisiasa na kuwa kigezo bora ambacho si tu kimebadilisha hatima ya taifa la Iran, lakini pia kimechora njia ya kupita Mapinduzi ya Kiislamu na vile vile kushuhudiwa harakati adhimu ya mwamko wa Kiislamu, ulimwenguni. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na kwa nini maadui wanaendelea kufanya njama dhidi ya taifa la Iran na kusema, lengo la maadui ni kuuzuia mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiendelee na harakati yake ya kimapinduzi inayozidi kupiga hatua. Amesema, hadi leo hii na ijapokuwa imeshapita miongo kadhaa tangu yalipotokea Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, lakini bado maadui wanatafuta kila njia hata za kupotosha fikra za Imam Khomeini na kujaribu kutia shaka katika msimamo wa kukabiliana na mabeberu aliokuwa nao Imam. Wakati ambapo katika kipindi chote cha mapambano yake, Imam Khomeini MA hakutaradadi wala kusita hata mara moja katika kufichua uovu wa mabeberu na kulaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, taifa la Iran kwa kushikamana na itikadi na fikra hizo za Imam Khomeini, limeendelea kupambana na dhulma na kushikamana vilivyo na njia yake hiyo iliyo wazi, kama ambavyo limeshikamana pia na msimamo wake usiotetereka wa kimapinduzi. Kwa hakika kushikamana na dafina na vielelezo hivyo vya Imam Khomeini MA ndiko kunakozifanya fikra za kisiasa na kimapinduzi za Imam Khomeini zizidi kuyatia nguvu Mapinduzi ya Kiislamu na kupata dhamana ya kufanikisha malengo makuu ya Jamhuri ya Kiislamu. Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akawataka watu wa matabaka yote na wafuasi wa fikra za Imam Khomeini wa kizazi cha leo na cha kesho, washikamane vilivyo na fikra hizo, licha ya kwamba wanaweza kulazimika kutoa gharama kubwa katika kulinda fikra hizo, kwani ni jambo la yakini kuwa, matunda na mafanikio ya kushikamana na fikra za Imam Khomeini MA na kuvumilia kwao ni makubwa zaidi.