Rais Raisi atilia mkazo wajibu wa kustawishwa uhusiano wa Iran na Pakistan
Rais Ibrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, nchi yake haina mipaka katika kustawisha uhusiano wake na Pakistan na kusisitiza kuwa, Iran ina uwezo wa kutosha wa kudhamini mahitaji muhimu ya Pakistan katika nyuga tofauti zikiwemo za mafuta, gesi na umeme.
Rais Raisi alisema hayo jana jioni wakati alipoonana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Bilawal Bhutto Zardari na huku akigusia uhusiano wa jadi wa mataifa haya mawili jirani ya Kiislamu na ambao ni wa karne nyingi na wa moyoni na wa kiitikadi, amesema kuwa, Iran na Pakistan si nchi jirani tu, bali ni ndugu wa damu.
Ameongeza kuwa, idadi kubwa ya watu kutoka nje ya Iran wanaofanya ziara katika Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash'had Iran ni kutoka Pakistan. Mapenzi ya wananchi wa Pakistan kwa Ahlul Bayt AS ni ya kupigiwa mfano, na hilo pekee limeandaa nyuga nzuri za kuzidi kukurubiana mataifa haya mawili ndugu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza tena kwa kusema, hakuna mipaka yoyote ya kustawishwa uhusiano wa Tehran na Islamabad na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kustawisha na kuimarisha uhusiano wake wa pande zote na Pakistan na kwamba Tehran ina nguvu na uwezo wa kutosha wa kuidhaminia Pakistan mahitaji yake katika maeneo tofauti yakiwemo ya mafuta, gesi na umeme.
Kwa upande wake, Bilawal Bhuto Zardari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameelezea kufurahishwa kwake na kupata fursa ya kuitembelea Iran na amesema: Mimi kwa kiwango kile kile cha kuwa kwangu mwana wa Pakistan, ni kwa kiwango hicho hicho pia mimi ni mwana wa Iran.