Iran yapinga mpango wa US kuunda mfumo wa ulinzi katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85732-iran_yapinga_mpango_wa_us_kuunda_mfumo_wa_ulinzi_katika_eneo
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeutaja mpango wa Marekani wa kutaka kuunda eti mfumo wa pamoja wa ngao ya makombora katika eneo hili kuwa ni wa kichochezi na kichokozi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2022 06:59 UTC
  • Iran yapinga mpango wa US kuunda mfumo wa ulinzi katika eneo

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeutaja mpango wa Marekani wa kutaka kuunda eti mfumo wa pamoja wa ngao ya makombora katika eneo hili kuwa ni wa kichochezi na kichokozi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Naser Kan'ani amesema matamshi ya maafisa wa Marekani ya kutaka kuundwa mfumo wa ulinzi katika eneo kwa kushirikiana na utawala haramu wa Israel na baadhi ya madola ya Kiarabu ni tishio kwa usalama wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu na usalama wa eneo zima la Asia Magharibi.

Amesema uundwaji wa mfumo wowote wa kiulinzi katika eneo utaenda kinyume na sera ya Jamhuri ya Kiislamu ya kupinga uwepo wa maajinabi katika eneo.

Kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Iran inapinga vikali njama za maadui za kutaka kuundwa eti NATO ya Asia Magharibi.

Kan'ani amesema mpango huo wa Marekani wa kutaka kuundwa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Asia Magharibi, utakaoshabihiana na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) unafanyika kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni.

Kombora la Khoramshahr la Iran

Kauli ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ni jibu kwa matamshi ya John Kirby, Mratibu wa Mawasiliano ya Kistratajia katika Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, ambaye hivi karibuni alizungumzia suala la kuundwa muungano huo wa kijeshi dhidi ya Iran.

Kirby alidai kuwa, Rais Joe Biden wa Marekani katika safari yake ya Saudia na katika ardhi za Palestina zilizopachikwa jina la Israel itakayofanyika baina ya Julai 13 na 16, atajadili na wenyeji wake juu ya 'tishio la Iran' na vilevile mikakati ya kuiwezesha Israel ipanue satua yake katika eneo.