Kan’ani Chafi: Hadaa ni sifa iliyoshamiri ya wanasiasa wa Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hadaa na kusema uongo ni sifa ya kawaida katika kauli za wanasiasa wa Marekani.
Kauli hiyo imekuja huku Joe Biden, Rais wa Marekani akiwa jana aliwasili katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina la Israel kwa lengo la kufanya mazungumzo na wakuu wa utawala wa Kizayuni na kisha aelekee Saudi Arabia.
Akiwa Saudia, Biden atafanya mazungumzo na viongozi wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambazo ni Saudi Arabia, Kuwait, Bahrain, UAE, Qatar na Oman. Hali kadhalika kikao hicho cha Jumamosi mjini Jeddah kitahudhuriwa na viongozi wa Iraq, Jordan na Misri.
Lengo la mkutano huo limetajwa kuwa ni kuzishinikiza nchi za Kiarabu ziwe na uhusiano wa karibu zaidi na utawala wa Kizayuni wa Israel sambamba na kushadidisha sera za chuki dhidi ya Iran katika eneo. Aidha kikao hicho kinatazamiwa kutumika kuishinikiza Saudi Arabia iongeze uzalishaji wa mafuta ya petroli.

Nasser Kan’ani Chafi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo ametuma ujumbe katika ukurasa wake wa Twitter kuhusu safari ya Biden huko Israel ambapo ameandamana na maafisa wake wa ngazi za juu akiwemo mshauri wa usalama wa taifa Jake Sullivan na kuandika: "Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa ameandamana na Biden mjini Tel Aviv ili kuipa nguvu ahadi ya Marekani kuwa itauunga mkono bila masharti utawala (wa Israel) unaoua watoto kwa wingi zaidi duniani."
Kan'ani ameendelea kusema kuwa, tokea mwanzo wa safari hiyo, Biden amekuwa akiituhumu Iran kuwa eti inaunga mkono mauaji ya watu wa Ukraine. Akisisitiza kuwa tuhuma hizo hazina msingi wowote, ameongeza kuwa, kusema uongo ni sifa iliyoshamiri ya wanasiasa wa Marekani. Aidha amesema wanasiasa hao wanapotosha ukweli kwa ajili ya kufikia malengo machafu.