Iran yazitaka Marekani na Aal Saud zifikirie upya siasa zao
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Hassan Firouzabadi amesema kuwa, viongozi wa Marekani na wale wa utawala wa Saudi Arabia wa Aal Saud waapaswa kufikiria upya siasa zao za kupenda vita na chokochoko dhidi ya mataifa ya Mashariki ya Kati.
Meja Jenerali Firouzibadi ameashiria matukio ya hivi karibuni katika eneo la Mashariki ya Kati na vitisho vya hivi karibuni vya utawala wa Aal Saud vya kutaka kutuma wanajeshi wake nchini Syria na kusema kuwa, kutokana na Saudia kushindwa mfululizo katika uga wa kisiasa, kiuchumi na hata katika siasa zake za kuunga mkono na kuyasaidia makundi ya kigaidi, hivi sasa imeshindwa na la kufanya huku Marekani ikiwa pamoja na Saudia katika siasa zake hizo kutokana na Washington na kukodolea macho visima vya mafuta ya bei rahisi. Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya kiislamu ya Iran amesema kuwa, hakuna Muislamu wa nchi za magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika ambaye amesalimika na njama za pembe tatu za Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia. Amesema, umefika wakati sasa kwa nchi za Kiislamu kuzinduka na kufikiria usalama, mamlaka ya kujitawala, uchumi na utamaduni wa wananchi wao.
Meja Jenerali Hassan Firouzabadi amebainisha kuwa, tishio la Saudia la kutuma wanajeshi wa cha nchi kavu huko Syria ni ishara ya kushindwa kwake kikamilifu katika uwanja wa vita dhidi ya Syria.