Iran ya Kiislamu imo kwenye maombolezo ya kufariki dunia Mtume Muhammad SAW
Iran ya Kiislamu hivi sasa imo kwenye maombolezo makubwa ya kukumbuka kufariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW na kuuawa shahidi mjukuu wake, Imam Hassan al Mujtaba AS ambaye ni Imam wa Pili wa Waislamu wa madhehebu ya Kishia.
Leo Jumapili, mwezi 28 Mfunguo Tano Safar, 1444 Hijria, inayosadifiana na tarehe 25 Septemba 2022 ni siku ya kukumbuka alipofariki dunia Bwana Mtume Muhammad SAW na alipouawa shahidi mjukuu wake kipenzi, Imam Hassan al Mujtaba AS.
Bwana Mtume Muhammad SAW alifariki dunia mwaka wa 11 Hijria baada ya kufikisha kwa uaminifu mkubwa na ufanisi wa hali ya juu ujumbe wa Uislamu aliotumwa na Mwenyezi Mungu kuwafikishia walimwengu akiwa ni rehema kwa viumbe wote.
Imam Hassan al Mujtaba AS aliuawa shahidi mwezi 28 Mfunguo Tano Safar mwaka wa 50 Hijria. Aliishi na baba yake kipenzi yaani Imam Ali AS kwa rakriban miaka 30. Imam Hassan al Mujtaba AS aliuawa shahidi akiwa na umri wa miaka 47 baada ya kupewa sumu na mkewe kwa amri ya Muawiya.
Siku za mwishoni mwa Mfunguo Tano ni siku za majonzi makubwa kwa wapenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW na Ahlul Bayt wake AS.
Leo kumbukumbu za misiba hiyo mizito katika ulimwengu wa Kiislamu zimefanyika kwenye miji mbalimbali ya Iran, huku Waislamu wa taifa hili wakitangaza kwa mara nyingine utiifu wao kwa Uislamu, Qur'ani na mafundisho matakatifu aliyokuja nayo Bwana Mtume Muhammad SAW.