Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran apongeza kuteuliwa mwenzake wa Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89412-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_iran_apongeza_kuteuliwa_mwenzake_wa_tanzania
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemnyooshea mkono wa tahania Stergomena Lawrence Tax, kwa kuteuliwa kuwa Waziri mpya wa Mashauri ya Kigeni wa Tanzania.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 18, 2022 07:54 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran apongeza kuteuliwa mwenzake wa Tanzania

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemnyooshea mkono wa tahania Stergomena Lawrence Tax, kwa kuteuliwa kuwa Waziri mpya wa Mashauri ya Kigeni wa Tanzania.

Katika ujumbe huo wa pongezi, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameipongeza serikali na taifa la Tanzania kwa ujumla, kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 tangu kuanzishwa uhusiano rasmi baina ya nchi mbili hizi.

Kadhalika amesema ana yakini kuwa uhusiano wa kirafiki na wa muda mrefu baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaimarishwa zaidi hususan katika nyuga za siasa, uchumi, sayansi na utamaduni na vile vile katika uga wa kimataifa.

Si vibaya kuashiria hapa kuwa, Agosti mwaka huu, Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliitembelea Tanzania ikiwemo Zanzibar na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Hassan Mwinyi.

Alisisitiza kuwa, uhusiano wa Iran na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unazidi kuwa imara. Aliashiria uwezo mkubwa wa Iran kiuchumi hasa katika nyuga za biashara, nishati, viwanda, teknolojia na vyuo vikuu na akatoa mwito wa kuondolewa vikwazo kwa mashirika na wafanyabiashara wa Iran nchini Tanzania hasa katika masuala ya visa. 

Waziri Abdollahian na Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa upande wake alitoa mwito wa kuimarishwa mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi baina ya Iran na Tanzania, mbali na kukubali mwaliko rasmi wa kuitembelea Iran kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi.

Mama Samia alisema, ana matumaini ya kufanya safari hiyo ya kuitembelea Iran kabla ya kumalizika mwaka huu wa 2022.