Iran yajibu uvumi wa gazeti la Marekani kuhusu kuishambulia Saudia
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amejibu uvumi ulioenezwa na gazeti la Marekani la Wall Street Journal lililodai kuwa kuna uwezekano Iran ikashambulia baadhi ya maeneo ya Saudi Arabia na kusema kuwa hayo ni madai chapwa yasiyo na msingi wowote.
Akijbu maswali ya waandishi wa habari, Nasser Kan'ani amesema, madai ya gazeti la Marekani la Wall Street Journal kwamba kuna uwezekano Iran ikashambulia baadhi ya maeneo ya Saudia ni madai ya uongo yasiyo na msingi wowote na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inahesabu uvumi wa namna hiyo unaonezwa na vyombo vya Magharibi na vya Kizayuni kuwa ni muendelezo tu wa uadui wa kila upande wa madola hayo dhidi ya taifa la Iran na lengo lake ni kuharibu mchakato chanya unaoendelea kwenye uhusiano wa nchi za eneo hili hivi sasa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inaendesha uhusiano wake kwa msingi wa kuheshimiana na kuchunga sheria za kimataifa. Siasa za kuishi kwa amani na usalama na majirani zake zinapewa kipaumbele kikubwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwani Tehran inaamini kuwa ukosefu wa utulivu na amani si kwa manufaa ya nchi yoyote katika eneo hili.
Juzi Jumanne, gazeti la Marekani la Wall Sreet Journal lilidai katika ripoti yake wakati huu wa kuharibika uhusiano wa Saudia na Marekani kwamba viongozi wa Saudi Arabia wamewapa taarifa viongozi wa Washington kuhusu uwezekano wa Iran kushambulia baadhi ya maeneo ya kiistratijia ndani ya ardhi ya Saudia.
Gazeti hilo lilidai pia kuwa, jeshi la Marekani na majeshi mengine yaliyopo Mashariki ya Kati yamewekwa kwenye hali ya tahadhari kubwa hivi sasa, masuala ambayo Iran inayahesabu kuwa ni muendelezo tu wa vita vya kisaikolojia vya Magharibi.