Qalibaf: Mkasa wa kuanguka ndege ya Ukraine ungali unatulemea mioyoni mwetu
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) ameashiria kutimia mwaka wa tatu tangu kujiri ajali ya ndege ya Ukraine na kueleza kuwa mkasa huo wa kuhuzunisha wa kuanguka ndege ya Ukraine ungali unatulemea mioyoni mwetu na kwa wananchi wa Iran kama ilivyokuwa siku ya kwanza.
Ndege aina ya Boeing 737 mali ya Shirika la Ndege la Kimataifa la Ukraine mnamo tarehe 8 Januari mwaka 2020 ilipokuwa ikitokea katika uwanja wa ndege wa Imam Khomeini (M.A) kuelekea Kyiv mji mkuu wa Ukraine ilianguka karibu na mkoa wa Tehran baada ya kupigwa na kombora la kikosi cha anga bila kukusudia ambapo abiria wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo walipoteza maisha.
Shirika la habari la IRNA limearifu kuwa, Muhammad Baqir Qalibaf Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema leo mwanzoni kwa kikao cha wazi cha majlisi kwamba anataraji kuwa, maombi ya kesi hii ya familia za wahanga wa ajali hiyo ya ndege inapaswa kujibiwa kwa mujibu wa sheria baada ya kumalizika mchakato wa ufuatiliaji wa mahakama na upelelezi; kesi ambayo inaendshwa kwa mujibu wa amri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa ushirikiano wa taasisi husika na familia za watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Wakati huo huo Qalibaf ameashiria kitendo cha jarida la Kifaransa ha kuwavunjia heshima na kuwatusi viongozi wa dini na wa kisiasa na kueleza kuwa utovu huo wa nidhamu wa jarida hilo la KIfaransa unaashiria ghadhabu ulizonazo mrengo wa Magharibi kutokana na kufeli kwa njama na mradi wao wa kuibua machafuko ya karibuni hapa nchini.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran wamestafidi na suhula na uwezo wao wote wa kisiasa, kiuchumi, kimataifa, kihabari na kiusalama lakini wananchi wa Iran licha ya mapungufu na matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wameilinda Jamhuri ya Kiislamu na kusambaratisha njama za maadui dhidi ya nchi yao."
Qalibaf amesema, hatua hizi zitaifanya azma ya wananchi wa Iran kuelekea kujitawala na maendeleo ya nchi kuwa na nguvu zaidi. Jarida la Charlie Hebdo linalochapishwa Ufaransa lilifanya kitendo cha kipuuzi na udhalilishaji kwa kuanzisha shindano la kimataifa la michoro ya vikaragosi ambapo lilichapisha picha za kuudhi zilizowatusi na kuwavunjia heshima viongozi wa kidini, matukufu ya Kiislamu, thamani za kidini na kitaifa za Waislamu ambapo katika makala yake maalumu iliyochapishwa tarehe nne mwezi huu wa Januari, lilichapisha picha za kukera sana pamoja na maneno yasiyostahili na ya matusi dhidi ya wanazuoni na viongozi wa kisiasa humu nchini.