Iran yatangaza kuwa tayari kusaidia kumaliza vita vya Ukraine
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amhakikishia mwenzake wa Russia Vladimir Putin kuhusu utayarifu wa Iran kuchukua jukumu chanya la mpatanishi katika kumaliza vita vilivyodumu kwa miezi 11 kati ya Russia na Ukraine.
Raisi aliwasilisha pendekezo hilo wakati wa mazungumzo ya simu na Rais Putin Jumatano ambapo amesema Iran iko tayari kuchukua jukumu kubwa na amilifu ili kumaliza uhasama na kuleta amani Ukraine ambayo ni Jamhuri ya Kisovieti ya zamani.
Pendekezo la Iran limekuja wakati, tangu kuanza kwa vita, washirika wa Magharibi wa Ukraine, wakiongozwa na Marekani, wamekuwa wakiipa nchi hiyo silaha za kiwango cha juu huku wakiiwekea Russia vikwazo vingi, hatua ambazo Moscow inasema zitaongeza tu mzozo huo.
Akifafanua zaidi, Rais wa Iran amesema masuala ya kikanda, ikiwa ni pamoja na yale yanayohusu eneo la Caucasus na Syria, yanaweza tu kutatuliwa kwa ushirikiano na uratibu.
Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu kila mara inasisitiza juu ya umuhimu wa kuimarishwa muungano wa kikanda na inasisitiza kuhusu athari mbaya ya uingiliaji wa kigeni katika eneo.
Kuhusiana na Syria, Rais wa Iran amesisitiza kuwa, masuala ambayo yanahusiana na nchi hiyo ya Kiarabu yanabidi yafuatiliwe kupitia Mchakato wa Astana. Iran na Russia, kama washirika wa serikali ya Syria, pamoja na Uturuki, ambayo iko upande wa upinzani, zilianzisha mchakato wa amani wa Astana mnamo Januari 2017 kwa nia ya kumaliza mzozo wa Syria kupitia ushiriki wa serikali ya Damascus na upinzani.
Kwingineko katika matamshi yake, Raisi amesisitiza ulazima wa kuendelezwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na Russia hususan katika maeneo ya usafiri na nishati.
Putin, kwa upande wake, amekaribisha pendekezo la Iran kuhusu kurejeshwa amani nchini Ukraine na vile vile kusisitiza umuhimu wa uratibu ndani ya Mchakato Astana kati ya pande husika katika utatuzi wa matatizo ya Syria.
Pia amesema ushirikiano wa kina wa kiuchumi kati ya nchi hizi una manufaa makubwa kwa mahusiano ya pande mbili.