Iran imejitosheleza katika uwanja wa teknolojia ya nyuklia
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ametangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejitosheleza katika uga wa teknolojia ya nyuklia.
Teknolojia ya nyuklia ni moja ya teknolojia za msingi ambayo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya teknolojia mpya na maendeleo ya viwanda vipya. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imegeukia matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia kwa kuegemea uwezo wa wataalamu wa ndani na imethibitisha kwa nia njema kwamba haina malengo mengine isipokuwa matumizi ya amani na viwanda ya nishati hiyo.
Katika miaka ya hivi karibuni, wanasayansi wa masuala ya nyuklia wa Iran wamefanikiwa kuzalisha aina mbalimbali za bidhaa za matumizi zinazohitajika na vituo vya kisayansi na utafiti nchini; Kwa mfano, wanasayansi wa Iran wamefanya uvumbuzi muhimu katika uwanja wa uchunguzi na matibabu ya saratani, ambayo itaingia katika hatua ya majaribio ya kliniki; Iran ni miongoni mwa nchi 5 bora duniani katika eneo hili.
Katika suala hili na kwa mujibu wa IRNA; Mohammed Eslami, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, alisema Jumatano katika hafla ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa shahidi wanasayansi wa nyuklia wa Iran, kwamba Iran imejitosheleza katika kutoa vifaa vilivyokuwa chini ya vikwazo na ina uwezo wa kusafirisha nje bidhaa hizo sasa." Ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo imekuwa nchi yenye uwezo kamili katika uga wa teknolojia ya nyuklia na imeweza kupata mafanikio makubwa kwa kutegemea nguvu za ndani."
Akizungumzia uwezo wa dawa za radiopharmaceuticals, Eslami amebainisha: "Uwezo tulionao katika dawa hizi za radiopharmaceutical umeifanya Iran kuwa moja ya nchi za kwanza duniani katika sekta hii."
Akizungumzia matumizi ya teknolojia ya nyuklia katika kutibu saratani, mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amebaini kuwa: "Athari za matibabu ya plasma ni kuzuia seli za saratani kutekeleza hujuma mwilini, na bila athari za chemotherapy, tiba ya plasma inaweza kukusanya na kusambaratisha seli zinazohusika katika kueneza saratani na hii ni hatua kubwa katika matibabu."