Al Zawawi asisitiza kuendelezwa Intifadha ya wananchi wa Palestina
(last modified Thu, 16 Jun 2016 07:23:44 GMT )
Jun 16, 2016 07:23 UTC
  • Al Zawawi asisitiza kuendelezwa Intifadha ya wananchi wa Palestina

Balozi wa Palestina nchini Iran amesema kuwa Intifadha ya wananchi wa Palestina itaendelea hadi kukombolewa Quds Tukufu.

Salah al Zawawi amesema kuwa Intifadha ya wananchi wa Palestina ilianza tangu miaka 100 iliyopita na itaendelea hadi kukombolewa kikamilifu Quds inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel. Amesema Intifadha imewatoa muhanga maelfu ya mashahidi kwa ajili ya Uislamu na kwa shabaha ya kukomboa Palestina na kwamba kwa msingi huo kwa sasa kuna udharura mkubwa zaidi wa kuwepo umoja huko Palestina kuliko wakati mwingine wowote ule. Balozi wa Palestina nchini Iran aliyasema hayo jana jioni katika mazungumzo na Ali Larijani Spika wa Majlisi ya Ushuari ya Kiislamu ya Iran yaani bunge pamoja na mabalozi wa nchi za Kiislamu hapa Tehran.

Salah Zawawi ameongeza kuwa Wazayuni wanafanya njama za kuzusha fitina na migawanyiko kati ya Waislamu na kwamba maadui wa Uislamu wana wawasiwasi na kuwepo muqawama huko Palestina.

Balozi wa Palestina ncini Iran amesema kuwa hali ya sasa katika Ulimwengu wa Kiislamu ni ya kusikitisha na kwamba nchi za Kiislamu hivi sasa zinazozana zenyewe kwa zenyewe na zimegawanyika kwa kadiri kuwa Ulimwengu wa Kiislamu unakabiliwa na mustakbali mbaya.