Amir-Abdollahian: SEPAH imeziokoa nchi za Ulaya na shari za Daesh/ISIS
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, nchi za Ulaya zina deni kwa jihadi kubwa iliyofanywa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika kupambana na ugaidi na kwamba miji mikuu ya nchi za Ulaya imebaki salama mbele ya shari ya mashambulizi ya magaidi wa Daesh (ISIS) kutokana na jihadi hizo kubwa ya SEPAH.
Shirika la habari la FARS limemnukuu Hossein Amir-Abdollahian akisema hayo katika mazungumzo ya simu na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Sweden, Tobias Billström, na huku akikosoa vikali hatua ya Bunge la Ulaya ya kuliweka jeshi la SEPAH katika orodha ya eti makundi ya kigaidi ameongeza kuwa, ana matumaini kwamba wakati huu ambapo Sweden ni mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya, umoja huo utafuata siasa za kimantiki za kuamiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Vile vile amesema, hatua haribifu ya Bunge la Ulaya dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH inakwenda kinyume na hati ya Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, Jeshi la SEPAH limefanya jihadi kubwa ya kupambana na magaidi wa Daesh katika nchi za Iraq na Syria na kwenye eneo hili la Asia Magharibi hadi lilipoliangamiza genge hilo la ukufurishaji na kuziokoa nchi za Ulaya na shari za mashambulizi ya genge hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Tobias Billström, amesema katika mazungumzo hayo ya simu kwamba wakati huu wa uwenyekiti wa nchi yake katika Umoja wa Ulaya, Sweden itajitahidi kuhakikisha kwamba uhusiano wa Iran na umoja huo unakuwa mzuri.
Amehimiza pia kufanyika mazungumzo ya kibalozi na kidiplomasia baina ya pande mbili na kusisitiza kuwa, pendekezo la hivi karibuni la Umoja wa Ulaya dhidi ya jeshi la SEPAH halina ulazima wowote wa kutekelezwa.