Admeli Fadavi: Jitihada za maadui za kuliyumbisha taifa la Iran zimefeli
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema njama za maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kutaka kuliyubisha taifa hili zimeshindwa na zitaendelea kushindwa.
Admeli Ali Fadavi amesema hayo leo Jumatano katika hafla iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Imam Hussein AS, kaskazini mashariki mwa Tehran na kueleza kuwa, kama zilivyogonga mwamba katika kipindi cha miaka 44 iliyopita, njama za maadui wa taifa hili kamwe hazitafua dafu.
Ameashiria fujo za hivi karibuni hapa nchini zilizochochewa na Wamagharibi wakiongozwa na Marekani na kusisitiza kuwa, "Hii si mara ya kwanza kwa maadui kufanya njama hizo, huko nyuma pia walifanya njama mbalimbali kama hizo lakini hawajawahi kufanikiwa hata mara moja."
Kamanda Fadavi amesema iwapo maadui watafanya kosa jingine lolote la kipumbavu dhidi ya Iran, basi Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali na la kuumiza.
Ameeleza bayana kuwa, maadui wa nchi hii hawajawacha hata siku moja kuchukua hatua za kiuadui na kiuhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu katika kipindi cha miongo minne iliyopita.
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la IRGC amegusia hatua ya Bunge la Ulaya ya kuiweka SEPAH katika orodha ye eti makundi ya kigaidi na kubainisha kuwa, maadui watashindwa pia kufikia malengo ya njama zao za kulitenga jeshi hilo na wananchi wa Iran, kama ambavyo wameshindwa pia katika njama zake nyingine zote.