Amir-Abdollahian: Shambulio katika ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan halikuwa la kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93386-amir_abdollahian_shambulio_katika_ubalozi_wa_jamhuri_ya_azerbaijan_halikuwa_la_kigaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amekanusha vikali kwamba shambulio dhidi ya ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan lilikuwa la kigaidi na akasema: "hatua hii imechochewa na sababu za kibinafsi tu".
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jan 27, 2023 23:41 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amekanusha vikali kwamba shambulio dhidi ya ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan lilikuwa la kigaidi na akasema: "hatua hii imechochewa na sababu za kibinafsi tu".

Katika shambulio lililofanywa jana Ijumaa na mtu mwenye silaha kwenye Ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan mjini Tehran, mkuu wa ulinzi wa ubalozi huo aliuawa na walinzi wengine wawili walijeruhiwa.
 
Katika maelezo yake ya awali aliyotoa, mshambuliaji huyo amesema alifanya shambulio hilo kwa sababu za binafsi.
 
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, baada ya kuwajulia hali majeruhi wa shambulio hilo la ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan, Amir-Abdollahian alifanya mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mkuu wa Hospitali ya Mashahidi ya Tajrish na balozi wa Jamhuri ya Azerbaijan mjini Tehran.
Aliyeshambulia ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan baada ya kutiwa mbaroni

Katika mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alieleza kwamba tangu mwanzo wa tukio hilo, Rais Ebrahim Raisi alitoa amri maalum ya ufuatiliaji wa kisheria, kimahakama na kiusalama, na akasema: mshambuliaji alikuwa na sababu za binafsi tu na vyombo vinavyohusika vinafuatilia kikamilifu kadhia hiyo.

 
Aidha amekanusha taarifa za kuhamishwa watu katika ubalozi wa Jamhuri ya Azerbaijan nchini Iran na akasema: tunafanya juhudi kuhakikisha kiwango cha mahusiano kinadumishwa, utulivu wa kinafsi katika mazingira ya ubalozi unarejeshwa na maamuzi mwafaka zaidi yanachukuliwa.
 
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Shahram Alamdari, mkuu wa Hospitali ya Mashahidi ya Tajrish, alisema, hali ya majeruhi wawili wa tukio hilo ni ya kuridhisha na akaongeza kuwa: wataalamu wote mabingwa wa huduma za ganzi, ugonjwa wa mifupa na upasuaji wa taya na sura kutoka hospitali nyingine za Tehran wamepelekwa hospitalini hapo ili kutoa huduma bora zaidi kwa majeruhi.
 
Kwa upande wake, Ali Alizadeh, Balozi wa Jamhuri ya Azerbaijan hapa mjini Tehran, ametoa shukrani kwa ufuatiliaji uliofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na kuwatembelea majeruhi hao na akaeleza kwamba hali za majeruhi ni nzuri.../