Rais wa Iran kuelekea China kwa ziara rasmi
Kwa kuitikia mwaliko rasmi wa Rais Xi Jinping wa China, rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ebrahim Raisi kesho Jumatatu anatazamiwa kuelekea mji mkuu wa China Beijing.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Rais Raisi ataondoka kuelekea mji mkuu wa China Beijing Jumatatu jioni akiongoza ujumbe wa ngazi za juu kwa ziara rasmi ya siku 3.
Katika safari hii, baada ya kukaribishwa rasmi na mwenzake wa China, rais kwanza atakuwa na mkutano wa faragha na Xi Jinping, na kisha kutakuwa mazungumzo ya wajumbe wa ngazi za juu wa nchi hizo mbili, pamoja na hafla ya kutiliana saini hati za ushirikiano ambayo itafanyika mbele ya marais hao mawili. Katika safari hii Raisi pia atashiriki katika mkutano wa pamoja wa wafanyabiashara na wanaharakati wa kiuchumi wa nchi hizo mbili na pia atakutana na Wairani wanaoishi nchini China. Mkutano na majadiliano na wanafikra na wasomi wakuu wa China itakuwa miongoni mwa mipango mingine ya rais mjini Beijing.
Mawaziri na maafisa wengine wa ngazi za juu wa serikali wataandamana na rais katika safari yake ya nchi hiyo. Rais wa Iran ndiye kiongozi wa kwanza wa kigeni kukutana na Rais wa China katika Mwaka Mpya wa China. Ikumbukwe kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China mwezi Machi mwaka 2021 zilitia saini mkataba wa ushirikiano wa miaka 25.
Mkataba huo unajumuisha ushirikiano katika sekta za kisiasa, kiusalama, kiulinzi, kiutamaduni, kilimo, kiuchumi, kisayansi, kitalii, mafuta na gesi, teknolojia ya habari na mawasiliano, biashara na afya.