Iran yavunja rekodi ya uzalishaji wa feleji duniani
Naibu wa Meneja Uzalishaji wa Shirika la Feleji la Mobarakeh la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inashikilia rekodi ya uzalishaji wa feleji duniani kutokana na hisa ya asilimia 34 ya shirika hilo.
Jumuiya ya Kimataifa ya Feleji imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, uzalishaji wa feleji ghafi duniani mwaka 2022 ulipungua kwa asilimia 4.3 ikilinganishwa na muda kama huo mwaka wa kabla yake. Lakini ripoti hiyo imesema, pamoja na kuwepo upungufu huo, uzalishaji wa feleji nchini Iran umeongezeka kwa asilimia 8 ambacho kilikuwa ni kiwango cha juu zaidi kati ya wazalishaji 10 bora wa feleji duniani mwaka huo.
Alireza Salimi, Naibu wa Meneja Uzalishaji wa Shirika la Feleji la Mobarakeh la Iran vile vile amesema, uzalishaji wa feleji ghafi nchini Iran katika kipindi hicho kilichotajwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Feleji cha mwaka 2022 ulikuwa ni tani milioni 30 na 600,000.
Amesema, kiwango kikubwa cha uzalishaji wa Shirika la Feleji la Mobarakeh kimeifanya Iran kuwa miongoni mwa nchi 10 bora zinazozalisha chuma na feleji kwa wingi duniani.
Vile vile amesema, kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mwaka 2022 eneo la Asia Magharibi lilizalisha tani milioni 44 za feleji ambapo Iran peke yake ilizalishaji asilimia 69.5 ya feleji za ukanda huu mwaka huo.
Naibu wa Meneja Uzalishaji wa Shirika la Feleji la Mobarakeh la Iran aidha amesema, katika hali ambayo mwaka jana 2022 nchi zote 10 kuu za zinazozalisha feleji duniani zilikuwa na upungufu wa asilimia 5 hadi 20 ya uzalishaji, ni Iran na India pekee ndizo zilizofanikiwa kuwa na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.