Mashindano ya 39 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu yafunguliwa rasmi mjini Tehran
Mashindano ya 39 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamefunguliwa rasmi Jumamosi alasiri mjini Tehran.
Sherehe za ufunguzi zimefanyika sambamba na sikukuu ya Idul Maba’ath (kuashiria kuteuliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) kama mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu).
Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Viongozi mjini Tehran na kuhudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa Iran ambapo pia walihutubu katika hafla hiyo.
Hujjatul Islam Seyed Mehdi Khamoushi, Mkuu wa Shirika la Masuala ya Wakfu na Misaada la Iran, ambalo limeandaa mashindano hayo, ametoa maelezo kuhusu mashindano ya mwaka huu, akibainisha kuwa hayo ni mashindano ya kwanza ambayo yanajumuisha kategoria ya Tarteel kwa wanawake.
Amesema kuwa jumla ya washiriki 52 kutoka nchi 33 watachuana katika fainali ya mashindano hayo mjini Tehran katika siku kadhaa zijazo.
Sherehe hiyo imeendelea kwa hotuba ya Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu Mohammad Mehdi Esmaeili.
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) Mohammad Baqer Qalibaf pia amehutubu akiwa kiongozi wa ngazi ya juu zaidi wa Iran aliyehudhuria ufunguzi wa mashindano hayo ya Qur’ani Tukufu.
Katika hotuba yake, amebainisha kuwa kuelewa mambo yaliyomo ndani ya Qur'ani Tukufu na kuyatekeleza kunaweza kuleta ustawi, elimu na maendeleo katika mataifa ya Kiislamu.

"Leo hii, umoja na mshikamano kati ya Waislamu ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote," amesisitiza na kuongeza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel hutekeleza njama za mara kwa mara za kuongeza hitilafu na migongano kati ya mataifa ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi.
Sherehe za kufunga mashindano hayo zimepangwa kufanyika Jumatano, Februari 22, huku Rais wa Iran Ebrahim Raeisi akitazamiwa kuhudhuria.
Kategoria za mashindano ya mwaka huu ya Qur’ani Tukufu ni pamoja na kuhifadhi, kusoma pamoja na tarteel kwa wanaume na kuhifadhi na tarteel kwa wanawake.
Jumla ya wasomaji na wahifadhi wa Qur'ani Tukufu 149 kutoka nchi 80 wakiwemo wanaume 114 na wanawake 35 walishiriki katika duru ya mchujo ambayo ilifanyika kwa njia ya intaneti.
Kauli mbiu ya toleo hili, kama lile lililotangulia, ni "Kitabu Kimoja, Umma Mmoja", jambo ambalo linaashiria Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa umuhimu mkubwa suala la umoja na udugu kati ya mataifa ya Kiislamu.
 
						 
						