Kamalvandi: Shutuma za IAEA dhidi ya Iran 'zimechochewa kisiasa'
(last modified Fri, 24 Feb 2023 07:59:28 GMT )
Feb 24, 2023 07:59 UTC
  • Kamalvandi: Shutuma za IAEA dhidi ya Iran 'zimechochewa kisiasa'

Ripoti zisizoisha za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) zinazotoa shutuma za uwongo na zisizo na msingi dhidi ya mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran "zina msukumo wa kisiasa" ili kuishinikiza nchi hii.

Hayo yamedokezwa na  Behrouz Kamalvandi msemaji Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) katika mahojiano maalum na Press TV.

Ameongeza kuwa IAEA hutangaza ripoti za siri kuhusu shughuli za nyuklia za Iran hata kabla ya uchunguzi kukamilika ili kuandaa mazingira ya uzushi dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.

Baada ya kukagua Kiwanda cha Kurutubisha Urani cha Fordow (FFEP) mwezi Januari, IAEA ilidai kuwa Iran imefanya "mabadiliko ambayo hayajatangazwa" kwenye muunganisho wa mashine za hali ya juu zinazorutubisha madini ya urani hadi kufikia asilimia 60 ya usafi kwenye kiwanda hicho.

Muda mfupi baadaye, taarifa ya pamoja ya Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani iliishutumu Iran kwa "kutokuwa thabiti katika kutimiza majukumu yake ya nyuklia."

Akitupilia mbali madai hayo yasiyo na msingi, Kamalvandi amesema Iran imebadilisha tu njia za kurutubisha, sio "mabadiliko yasiyotangazwa kwenye taarifa za muundo" (DIQ) kama ilivyoelezwa na IAEA.

Kamalvandi aliongeza kuwa baada ya shirika hilo kufahamishwa kuhusu "kosa" la mkaguzi, alirudi kwa ukaguzi mwingine na kuthibitisha kuwa Iran haijafanya mabadiliko yoyote kinyume cha sheria.

Kamalvandi alikashifu kauli ya Marekani na washirika wake wa Ulaya kama hatua "iliyopangwa".

Akizungumzia ripoti ya hivi majuzi ya Bloomberg iliyodai kuwa IAEA "inajaribu kufafanua jinsi Iran ilivyokusanya madini ya urani iliyorutubishwa hadi asilimia 84," msemaji wa wakala wa shirika la nyuklia la Iran alisema kupata chembechembe za urani zilizorutubishwa kwa kiwango cha juu kwenye mabomba yanayounganisha mashinepewa ni "suala la kawaida."

Kamalvandi pia ameikosoa IAEA kwa kuruhusu mawasiliano kati ya Tehran na shirika hilo kuvuja katika vyombo vya habari, na kushikilia wakala "hatia kwa asilimia 100" katika kesi hiyo.

Msemaji wa Shirika la Nyuklia la Iran amesisitiza kwamba kuwa na teknolojia ya nyuklia ni lazima kwa nchi kama Iran yenye idadi kubwa ya watu milioni 80 kwani teknolojia hii inaweza kukidhi mahitaji yake ya matibabu.

Afisa huyo amebainisha kuwa Iran lazima iwe na uwezo wa kuzalisha umeme usio na uchafuzi wa mazingira kama vile umeme wa nyuklia, kwani usambazaji wa umeme kwa kutumia maji nchini Iran hauwezi kutegemewa tena kutokana na uhaba wa mvua.

Ameongeza kuwa teknolojia ya nyuklia inaweza kunufaisha viwanda vingine vikubwa vikiwemo vya kuchimba mafuta na kampuni za saruji.

 

Tags