Kamalvandi: Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kutembelea Tehran karibuni hivi
-
Behrouz Kamalvandi
Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema kuwa: "Makamu wa Rais na Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Muhandisi Mohammad Eslami amemwalika rasmi Bw. Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kuitembelea Iran siku zijazo.
Shirika la habari la Tasnim, limemnukuu Behrouz Kamalvandi, msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran akisema: "Katika siku zilizopita, kulifanyika mazungumzo mazuri na ya kutia matumaini kati ya Iran na ujumbe wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ulioongozwa na Massimo Apparo."
Amefafanua zaidi kwa kusema, ziara ya Grossi nchini Iran itafanyika karibuni hivi. Maelezo zaidi kuhusu ziara hiyo yatatolewa kwa vyombo vya habari hivi karibuni.
Siku chache zilizopita pia, Kamalvandi aliulaumu Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa tuhuma za uwongo na zisizo na msingi dhidi ya mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa, tuhuma hizo zimetolewa kisiasa.
Aliulaumu wakala wa IAEA kwa kutangaza ripoti za siri kuhusu shughuli za nyuklia za Iran hata kabla ya uchunguzi kukamilika na kusema kuwa, wakala huo unafanya hivyo ili kuandaa mazingira ya uzushi dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian amefanya ziara mjini Geneva Uswiswi na kusema katika mazungumzo yake na waziri mwenzake wa Finland kuwa, ana matumaini ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA mjini Tehran itaongeza kasi ya mazungumzo kuhusu masuala ya kiufundi ya JCPOA.