ICJ: Marekani ilikiuka sheria ya kimataifa kuzuia mali za Iran, iilipe fidia
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) yenye makao yake mjini The Hague wamehukumu kuwa Marekani ilikiuka sheria za kimataifa kwa kuziruhusu mahakama za nchi hiyo kutaifisha mali zenye thamani ya takribani dola bilioni mbili kutoka kwa makampuni ya Iran, na kuiamuru Washington ilipe fidia, kiwango ambacho kitafahamika hapo baadaye.
Katika uamuzi iliotangaza jana Alkhamisi, ICJ ilisema hatua ya Washington ya kuzuia fedha za watu na makampuni kadhaa ya Iran, ikiwa ni pamoja na dola bilioni 1.75 kutoka Benki Kuu ya Iran (CBI), "ni wazi kabisa haiingii akilini".
Mahakama hiyo, hata hivyo, ilisema haina mamlaka ya kutoa uamuzi juu ya ufungiaji wa mali za Benki Kuu ya Iran.
Kufuatia kutangazwa uamuzi huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema hukumu hiyo inadhihirisha uhalali wa misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu na mienendo haramu ya Marekani.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema: "kwa mujibu wa uamuzi huo muhimu, mahakama imetupilia mbali utetezi usio na uthibitisho wa Marekani na kuitambua Iran kama upande wenye haki kwa kusisitiza kuwa Washington imehalifu kutekeleza wajibu wake. Wajibu wa Marekani wa kufidia hasara hiyo itakuwa sababu ya busara zaidi ya uhalali wa ombi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran".
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa, kwa upande wake: "inachukulia kama moja ya wajibu wake wa asili kushinikiza kupatikana haki za taifa la Iran, na itatumia njia na taratibu zote za kidiplomasia, kisheria na kimahakama kudai haki za wananchi waheshimika wa Iran na maslahi ya taifa la Wairan".
ICJ, ambayo inajulikana pia kama Mahakama ya Dunia, ni mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia mizozo kati ya nchi. Japokuwa hukumu zinazotolewa na ICJ ni wajibu kutiiwa, lakini mahakama hiyo haina uwezo wa kulazimisha zitekelezwe.../