Rais wa Iran: Mataifa ya Kiislamu lazima yakabiliane na ukatili wa Israel
Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema nchi za Kiislamu lazima ziungane na kukabiliana na ukatili wa utawala wa Israel dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina.
Raisi aliyasema hayo jana Jumapili katika mkutano na Hicabi Kırlangıç, balozi mpya wa Uturuki mjini Tehran, na kuongeza kuwa: "Mataifa ya Kiislamu yanawataka watawala kukabiliana na uhalifu wa utawala wa Kizayuni (Israel) dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Palestina."
"Kwa hiyo, ni muhimu kwa nchi za Kiislamu kuwa na mipango ya kukabiliana na ukatili wa Israel."
Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, Israel imeongeza mashambulizi katika miji na vijiji vya Palestina katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu. Kutokana na mashambulizi hayo makumi ya Wapalestina wameuawa na wengine wengi kukamatwa.
Mashambulizi mengi yamelenga Nablus na Jenin, ambapo vikosi vya jeshi la Israel vimekuwa vikijaribu kuzuia kuongezeka kwa oparesheni za wanamapambano wa Palestina dhidi ya Wazayuni maghasibu.
Mashambulio hayo yameongezeka sana katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, huku wanajeshi wa Israel wakivamia mara kwa mara Msikiti wa al-Aqsa katika eneo la Quds inayokaliwa kwa mabavu, na kuwapiga waumini wa Kipalestina kabla ya kuwakamata.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kimataifa yamelaani matumizi ya nguvu kupita kiasi ya Israel na "sera ya kuwafyatulia risasi" Wapalestina.
Kwingineko katika hotuba yake, Raisi ameashiria uhusiano uliokita mizizi kati ya Iran na Uturuki na kusema: "Licha ya juhudi zinazofanywa na watu wenye nia mbaya, kuna ulazima wa kutegemea mambo ya pamoja ya kidini na kiutamaduni na kufanya kazi kwa ajili ya kuzidisha na kupanua uhusiano kati ya nchi za Kiislamu katika nyanja mbalimbali."
Balozi mpya wa Uturuki, ambaye aliwasilisha hati zake kwa Rais Ebrahim Raisi, alisema nchi yake inafurahia uhusiano mzuri na Iran. Ameahidi kufanya juhudi kubwa kuboresha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na kuongeza mawasiliano na maingiliano kati ya pande hizo mbili.