Kiongozi: Umma ufahamishwe kuhusu hiana ya Marekani katika mapatano ya nyuklia
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa umma unapaswa kufahamishwa kuhusu hiana inayofanywa na Marekani katika utekelezwaji wa mapatano ya nyuklia yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo Jumatatu usiku mjini Tehran alipokutana na malenga mashuhuri na maustadh wa fasihi ya Kifarsi katika mkesha wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Hassan Mujtaba AS. Aidha katika kikao hicho walikuwemo malenga wa Kifarsi kutoka Pakistan, India na Afghanistan.
Akizungumza katika kikao hicho, Ayatullah Khamenei amesema kuweka wazi hiana ya Marekani katika kutekeleza ahadi zake kuhusu mapatano ya nyuklia ni kati ya maudhi zinazoweza kuwepo katika utunzi wa mashairi. Ameongeza kuwa, mbali na wanasiasa, wasanii na hasa malenga wanapaswa kuufahamisha umma kuhusu hiana hiyo ya Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "Leo vita ni vita laini na kuna mapambano ya kisiasa na kiutamaduni yanayoendelea." Amesema malenga wanapaswa kuwa na nafasi yenye taathira katika kutekeleza majukumu yao. Kiongozi Muadhamu amesisitiza umuhimu wa kushajiishwa utungaji na usomaji mashairi hai katika maudhui muhimu kama vile Palestina, Yemen, Bahrain, kujihami kutakatifu, mashahidi wapiga mbizi, mashahidi walinzi wa Haram Takatifu za Kizazi cha Mtume SAW na pia mashairi kuhusu kudhulumiwa mujahidina kama vile Sheikh Zakzaky, mwanazuoni aliyedhulumiwa, shujaa na mwenye irada kutoka Nigeria. Kiongozi Muadhamu pia amesisitiza kuhusu kutarjumiwa mashairi yenye maudhui za Palestina, kujihami kutakatifu na Yemen pamoja na maudhui zingine za eneo.