Iran kuzindua safari za ndege za kila wiki kwenda Saudi Arabia
(last modified Mon, 24 Apr 2023 07:06:20 GMT )
Apr 24, 2023 07:06 UTC
  • Iran kuzindua safari za ndege za kila wiki kwenda Saudi Arabia

Iran ina mpango wa kuzindua safari za ndege za abiria kila wiki kwenda Saudi Arabia kufuatia ombi rasmi kutoka kwa wakuu wa Saudia huku kukiwa na uboreshaji wa uhusiano wa nchi hizi mbili jirani.

Waziri wa Usafiri wa Iran, Mehrdad Bazrpash, alisema jana Jumapili kwamba viongozi wa Saudia wameiomba Iran kuanzisha safari za ndege za abiria mara tatu kwa wiki kwenda katika nchi hiyo.

Bazrpash amesema safari hizo za ndege zitazinduliwa hivi karibuni na ameongeza kwamba hazijumuishi mipango iliyopo kati ya nchi hizo mbili kuhusu ndege zinazowabeba mahujaji wa Irani kwenda kwenye kutekeleza ibada ya Hajj nchini  Saudia kila mwaka

Waziri huyo ameeleza kuwa, kuanzishwa safari hizo za ndege za kila wiki baina ya Iran na Saudi Arabia, pamoja na safari za ndege za Mahujaji ni ishara ya kupanuka uhusiano wa nchi mbili.

Tangazo hilo linakuja wakati wa mipango ya Iran na Saudi Arabia kufungua tena balozi na kurejesha uhusiano wa kidiplomasia miaka saba baada ya nchi hizo mbili kukata uhusiano wao rasmi.

Mpango huo unafuatia makubaliano yaliyofikiwa kwa upatanishi wa China mapema Machi ambayo yalisema kwamba nchi hizo mbili za Kiislamu zinapaswa kufungua tena balozi zao  ifikapo Mei 9.

Wataalam wanasema mapatano ya kuboresha uhusiano kati ya Iran na Saudi Arabia yanaweza kufungua njia ya upanuzi mkubwa wa uhusiano wa kiuchumi na biashara kati ya nchi hizo mbili za Kiislamu.

Tags