Iran: Tunapinga kuendelea vita nchini Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i96720-iran_tunapinga_kuendelea_vita_nchini_ukraine
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inapinga vita vya Ukraine na inaunga mkono juhudi za kusimamishwa vita na kurejea usalama na amani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 27, 2023 05:38 UTC
  • Iran: Tunapinga kuendelea vita nchini Ukraine

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inapinga vita vya Ukraine na inaunga mkono juhudi za kusimamishwa vita na kurejea usalama na amani nchini humo.

Nasser Kan'ani amesema hayo baada ya gazeti la Marekani la Wall Street Jounal kutoa madai yasiyo na msingi ya kwamba eti Tehran imeipelekea silaha Russia kupitia bahari ya Caspian. 

Madai hayo ya uongo ya gazeti la Marekani yametolewa katika hali ambayo, tangu ulipoanza mgogoro wa Ukraine, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran muda wote imekuwa ikipinga vita hivyo na imekuwa ikikanusha vikali madai yasiyo na mashiko, yanayotolewa na madola ya Magharibi hasa Marekani kwamba inaipa silaha Russia za kutumika kwenye vita vya Ukraine.

Nchi za Magharibi zinaisheheneza silaha Ukraine halafu zinazituhumu nchi zisizohusika kuchochea vita hivyo

 

Usiku wa kuamkia leo Alkhamisi, Nasser Kan'ani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa mara nyingine amekanusha madai hayo katika majibu yake kwa mwandishi wa shirika la habari la FARS aliposema, madai ya gazeti la Marekani la Wall Street Journal ya kwamba Iran imeipelekea silaha Russia kupitia bahari ya Caspian, hayana msingi wowote.

Amesema, madola ya Magharibi ndiyo yanayoendelea kuimiminia silaha Ukraine na kuchochea zaidi moto wa vita lakini wakati huo huo madola hayo yanajipa uthubutu wa kuzituhumu nchi nyingine zisizohusika na vita hivyo na kueneza habari za uongo ili kufunika jinai na siasa zao za kuchochea moto wa vita huko Ukraine.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran vile vile amesisitiza kuwa, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu uko wazi kuhusu vita vya Ukraine, tunapinga vita hivyo na tunaunga mkono amani na usimamishaji vita nchini humo.