Kwa nini makubaliano yoyote na Iran ni fedheha kwa Trump?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i138726-kwa_nini_makubaliano_yoyote_na_iran_ni_fedheha_kwa_trump
Kadiri uwezekano wa kufikiwa makubaliano kati ya Marekani na Iran unavyoongezeka, waandishi wa habari na wachambuzi mashuhuri wa Marekani wanatoa maoni yao kwa uwazi zaidi kuhusu kushindwa Trump na Netanyahu kutimiza matakwa yao katika mashambulio ya kijeshi dhidi ya Iran.
(last modified 2026-05-29T12:45:03+00:00 )
May 29, 2026 12:41 UTC
  • Trump
    Trump

Kadiri uwezekano wa kufikiwa makubaliano kati ya Marekani na Iran unavyoongezeka, waandishi wa habari na wachambuzi mashuhuri wa Marekani wanatoa maoni yao kwa uwazi zaidi kuhusu kushindwa Trump na Netanyahu kutimiza matakwa yao katika mashambulio ya kijeshi dhidi ya Iran.

Robin Wright, mwandishi wa habari mkongwe wa Asia Magharibi, ameelezea katika gazeti la New Yorker "Operesheni ya Epic Fury" ya utawala wa Trump dhidi ya Iran kama "Maafa makubwa." Operesheni hiyo ilianza kwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni mnamo Februari 28, na kuahidi kuharibu kabisa mpango wa nyuklia wa Iran, kukata uungaji mkono wa Tehran kwa mrengo wa muqawama katika eneo, na hata kubadilisha mfumo wa utawala wa Iran.

Lakini baada ya uvamizi huu wa kijeshi wenye gharama kubwa, matokeo ya mwisho yamekuwa kinyume na malengo hayo makubwa, ambapo mazungumzo ya sasa yanaelekea kwenye makubaliano dhaifu zaidi kuliko alivyotarajia Trump.Thomas Friedman, mwandishi mashuhuri wa gazeti la New York Times, pia ametilia shaka mtazamo wa rais wa Marekani kuhusu vita na Iran kwa sauti ya ukosoaji na kuukejeli katika makala yenye kichwa cha habari kinachosomeka "Bwana Trump, Hii Ndio Ladha Chungu ya Kushindwa, na sio Karamu ya Ushindi," ambapo amesisitiza kwamba hata kama Marekani itafanikiwa kuharibu urani ya Iran iliyorutubishwa, lakini sehemu ya mpango wa nyuklia na uwezo wa Kistratijia wa Iran utaendelea kuwepo na kwamba mfumo wake wa kisiasa hautabadilika.

Suala ambalo, mwandishi anasema kuwa, linaweza kupelekea kuimarika zaidi nafasi ya Tehran kieneo na kimataifa. Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, sehemu ya matokeo ya mzozo huu yatakuwa makubaliano ya siku za usoni ambayo yanaweza kupunguza hatua kwa hatua baadhi ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran, kuipa Tehran rasilimali zaidi za kifedha na hivyo kuongeza nguvu zake katika eneo.

Sehemu nyingine ya uchambuzi huu inabainisha hatari zisizotarajiwa za vita na kueleza kuwa Washington na Tel Aviv hazikuzingatia kikamilifu hali zinazoweza kutokea kabla ya mzozo kuanza, ikiwa ni pamoja na uwezo wa Iran wa kuvuruga njia muhimu za nishati, likiwemo Lango-Bahari la Hormuz, ambapo sehemu kubwa ya biashara ya mafuta duniani hupitia.Dani Citrinovich, mchambuzi mkuu wa Asia Magharibi na mtafiti katika Baraza la Atlantiki amesisitiza katika mahojiano na gazeti la New Yorker kwamba, makubaliano yoyote yanayoweza kufikiwa na Iran yatakuwa fedheha na kushindwa kistratijia kwa Donald Trump, na kwamba kampeni ya kijeshi ya Washington na Tel Aviv imeshindwa kubadilisha mahesabu ya Tehran, kwa kadiri kwamba White House sasa haina budi ila kukubali masharti ya upande wa pili.

Mchambuzi huyo anasisitiza kuwa, kinyume na lengo la awali la jeshi la Marekani na Israel la kutaka kuupindua utawala wa Iran, kampeni hii ya kijeshi hatimaye imepelekea kuimarika zaidi utawala huo. Ingawa vita vinaweza kuwa na mafanikio ya kimbinu, lakini vimekuwa kushindwa wazi kimkakati kwa Washington. Kinyume na dhana ya Ikulu ya White House, Citrinovich anaamini kuwa milipuko ya mabomu, mzingiro na kushambuliwa vituo vya nishati vimeshindwa kuilazimisha Tehran ijisalimishe, ambapo viongozi wa Iran kwa kudiriki vizuri kuwa hivi ni vita vya kufa na kupona, wametumia nguvu zao zote kukabiliana na adui na sasa, wakiwa na nguvu kubwa, hawakubali tena matakwa ya kubomoa taasisi zao za nyuklia.

Dani Citrinovich pia anaamini kwamba rais wa Marekani amenasa kati ya chaguo baya na baya zaidi na sasa analazimika kukubali mapatano mabaya kabisa kutokana na hofu ya kuongezeka mivutano, hofu ya kutuma askari wa nchi kavu, na wasiwasi kuhusu gharama za kiuchumi za vita kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula.Kwa mujibu wa mchambuzi huyu, makosa makubwa zaidi yaliyofanywa na Washington ni kuishinikiza Iran na kuilazimu itumie wenzo wake muhimu zaidi wa nguvu katika kudumaza uchumi wa dunia, kwa kufunga Lango-Bahari la Hormuz, chombo cha nguvu ambacho mafanikio yake yamewashangaza wengi ulimwenguni. Iran sasa inatumia chombo hicho kama wenzo muhimu wa kufikia mapatano na hasimu wake kwenye meza ya mazungumzo.

Vita hivi vimesambaratisha kabisa itikadi ya Netanyahu, ambaye kila mara alikuwa akiahidi kuwa kwa ushirikiano na uungwaji mkono kijeshi wa Marekani, angeishinda Iran mara moja. Katika upande wa Lebanon pia, ikiwa Trump anataka kufikia makubaliano ya kudumu, itamlazimu afunge kabisa mikono ya Netanyahu katika utekelezaji wa jinai zake dhidi ya Hizbullah. Ni wazi kuwa uamuzi wa Trump wa kujiondoa katika mapatamo ya nyuklia ya JCPOA bila ya kuwa na stratijia mbadala umetajwa kuwa makosa makubwa zaidi ya kistratijia katika historia.

Mahojiano ya gazeti la New Yorker na Citrinovic yanahitimisha kwamba makubaliano yoyote yanayoweza kufikiwa sio ishara ya ushindi kwa Trump, bali ni jaribio la kujiondoa kwa heshima katika vita ambavyo havikufikia malengo yake ya awali, na isitoshe, vimebadilisha mlingano wa nguvu kwa maslahi ya Iran. Katika kujibu swali kuhusu namna wanahistoria wa siku za usoni watakavyolichukulia tukio hili, John Mearsheimer, mwananadharia mashuhuri wa Marekani anasemaa: Wakati Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Marekani, lilipowauliza wanahistoria wa diplomasia huko New York, yapata miaka miwili iliyopita kuhusu Ili kubaini kosa kubwa zaidi la sera ya mambo ya nje ya Marekani, walisema ni Vita vya Iraq vya mwaka 2003. Lakini ninaamini kwamba shambulio la Iran mnamo Februari 28 litaingia katika vitabu vya historia kama kosa kubwa zaidi la sera za kigeni lililowahi kufanywa na Marekani, na hivyo kuibua tofauti kubwa vikilinganishwa na vya Iraq.