Mkuu wa WHO atembelea Bunia, kitovu cha Ebola asema , tuko pamoja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138760-mkuu_wa_who_atembelea_bunia_kitovu_cha_ebola_asema_tuko_pamoja
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema imani ya jamii itakuwa jambo muhimu katika kudhibiti mlipuko wa Ebola unaoendelea kusambaa kwa kasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
(last modified 2026-05-31T02:58:40+00:00 )
May 31, 2026 02:53 UTC
  • Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom  akiwa mjini Bunia, katika eneo la mashariki mwa DRC 30 Mei, 2026.
    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom akiwa mjini Bunia, katika eneo la mashariki mwa DRC 30 Mei, 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema imani ya jamii itakuwa jambo muhimu katika kudhibiti mlipuko wa Ebola unaoendelea kusambaa kwa kasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ameyasema hayo Jumamosi wakati timu za afya zikiharakisha juhudi za kukabili dharura hiyo ambayo tayari imeenea katika majimbo kadhaa na kuvuka mpaka hadi Uganda.

Akizungumza mjini Bunia, mji mkuu wa Jimbo la Ituri na kitovu cha mlipuko huo, mashariki mwa nchi, Tedros amesema jamii za wenyeji lazima ziwe kiini cha mwitikio dhidi ya aina ya Ebola aina ya ya Bundibugyo, ambayo kwa sasa haina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa.

Kufikia tarehe 27 Mei 2026, jumla ya wagonjwa 906 wanaoshukiwa kuwa wa Ebola na vifo 223 vinavyoshukiwa kuhusiana na ugonjwa huo vilikuwa vimeripotiwa nchini DRC. Katika DRC na Uganda kwa pamoja, visa 134 vilivyothibitishwa na vifo 18 vilivyothibitishwa vilikuwa vimeripotiwa kufikia tarehe 29 Mei.

Tedros ametumia ziara yake kukutana na maafisa wa serikali, viongozi wa jamii, mashirika ya kibinadamu na washirika wa afya, akisisitiza kuwa imani ya wananchi na ushiriki wa jamii vitakuwa muhimu katika kukomesha maambukizi.

Ameeleza matumaini ya kukutana na vikundi vya wanawake, viongozi wa dini, wawakilishi wa wafanyabiashara na vijana wakati wa ziara yake, akieleza kuwa kujenga imani ni mchakato unaoanza kwa kusikiliza.

Wakati huo huo, juhudi za kukabiliana na mlipuko zinaendelea kuimarishwa.

WHO imewasilisha zaidi ya vifaa 2,000 vya uchunguzi wa maabara na kusaidia kuimarisha uwezo wa uchunguzi katika vituo muhimu vya usafiri. Shirika hilo pia linaimarisha mifumo ya maji katika vituo vya matibabu ya Ebola ili kusaidia kuzuia na kudhibiti maambukizi.

 

Hata hivyo, kuna wasiwasi mkubwa kuwa mlipuko huo unaweza kuvuruga huduma nyingine muhimu za afya katika maeneo yaliyoathirika.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi, UNFPA, limesema vituo vya afya vinaendelea kuelekeza wafanyakazi, vifaa na miundombinu katika shughuli za kukabiliana na Ebola, jambo ambalo limepunguza upatikanaji wa huduma kama upasuaji wa dharura wa kujifungua, huduma za watoto wachanga, uzazi wa mpango na huduma za baada ya kujifungua.

Ili kusaidia kuendelea kwa huduma hizo, UNFPA inapeleka wakunga, vifaa vya afya ya uzazi na vifaa tiba huku ikiunga mkono mpango wa kikanda wa mwitikio unaozihusisha DRC, Uganda na South Sudan.

 Tedros amesema mwitikio huo lazima uende zaidi ya kukabiliana na mlipuko wa sasa pekee.

 “Tunapopambana na mlipuko huu pamoja nanyi, tumejizatiti kuhakikisha kuwa huduma nyingine muhimu za afya na misaada ya kibinadamu zinaendelea kutolewa kwa jamii za Ituri na maeneo mengine,” amesema.

Pia Ameeleza imani yake kuwa mlipuko huo unaweza kudhibitiwa.

 “DRC imekabiliwa na Ebola mara 16 hapo awali na imefanikiwa kukomesha kila mlipuko,” amesema. “Huu ni wa 17. Historia hiyo inanipa matumaini makubwa.”

Akihitimisha hotuba yake, Tedros alitaka kuwapa matumaini wananchi walioathirika.

“Hamko peke yenu katika hili,” amesema. “Tupo hapa, tuko pamoja nanyi, na tutalivuka jambo hili kwa pamoja.”