Iran yasema mapatano na Marekani bado hayajafikiwa, yakataa mabavu ya Trump
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i138754-iran_yasema_mapatano_na_marekani_bado_hayajafikiwa_yakataa_mabavu_ya_trump
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Ijumaa kwamba mabadilishano ya ujumbe kati ya Iran na yanaendelea, lakini hadi sasa hakuna mwafaka wa mwisho uliofikiwa huku akisisitiza kuwa Tehran haikubali lugha ya mabavu.
(last modified 2026-05-30T11:03:08+00:00 )
May 30, 2026 11:01 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei
    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Ijumaa kwamba mabadilishano ya ujumbe kati ya Iran na yanaendelea, lakini hadi sasa hakuna mwafaka wa mwisho uliofikiwa huku akisisitiza kuwa Tehran haikubali lugha ya mabavu.

Esmaeil Baghaei amesema katika mahojiano na televisheni ya taifa ya Iran kwamba: “Tuliagana na lugha ya mabavu miaka 47 iliyopita.” Ameongeza kusema: “Hakuna dola lolote la Magharibi linaloweza kutumia lugha ya ‘kulazimisha’ katika mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunafanya maamuzi yetu wenyewe kwa kuzingatia maslahi na haki za taifa la Iran.”

Kauli zake zilikuja saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kudai kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social kwamba lazima usimamizi wa Iran katika Mlango wa Hormuz uondolewa. Pia alidai kwamba uamuzi kuhusu makubaliano na Iran utachukuliwa hivi karibuni.

Iran ilifunga Mlango wa Hormuz kwa maadui zake na washirika wao baada ya kuanza vita vya kichokozi vya Marekani na Israel dhidi yake tarehe 28 Februari na kuendelea kwa siku 40. Mamlaka za Iran zilianza kutekeleza udhibiti mkali zaidi mwezi uliopita kufuatia tangazo la Trump kuhusu kutekelezwa mzingiro uliolenga meli na bandari za Iran.

Iran imesema hatua hizo za Trump zinakiuka masharti ya usitishaji mapigano na kwamba baadaye ziliongezwa kwa upande mmoja na Washington.

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, yanayosimamiwa na Pakistan na kuratibiwa na Qatar, yanaendelea kwa msingi wa pendekezo la vipengele 14 la Jamhuri ya Kiislamu. Lengo lake ni kufikiwa kwa hati ya makubaliano ya kumaliza vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, kusitishwa uhasama wa Marekani baharini, na  kuachiliwa kwa mali za Iran zilizozuiwa.

Baghaei amesisitiza kwamba Mlango wa Hormuz uko ndani ya maji ya kieneo ya Iran na Oman na hivyo ni nchi hizo mbili jirani zitakzoamua kuhusu usimamizi wa eneo hilo.