Iran yasema uingiliaji wa kigeni nchini Sudan 'unatia wasiwasi sana'
-
Hossein Amir-Abdollahian
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasema hatua ya baadhi ya nchi kuingilia masuala ya ndani ya Sudan imechangia hali ya sasa ambayo inatia wasiwasi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa: "Hali ya Sudan inatia wasiwasi sana. Ikiwa hatua zinazofaa hazitachukuliwa, umoja wa mipaka ya Sudan utakuwa hatarini na hilo litakuwa na athari katika eneo hilo la Afrika"
Ameelezea masikitiko yake juu ya uingiliaji wa madola ajinabi na uchochezi wao nchini Sudan, akihimiza mazungumzo ya ndani na maelewano kwa ajili ya kutatua mgogoro huo.
Mapigano makali yalizuka Aprili 15 kati ya kiongozi mkuu wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye anaongoza jeshi la kawaida, na naibu wake aliyegeuka mpinzani Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, ambaye anaongoza Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema takriban raia 551 wameuawa hadi sasa na wengine karibu 5000 wamejeruhiwa, lakini idadi halisi huenda ikawa juu kutokana na ugumu wa kupata vituo vya matibabu.
Ghasia hizo zimepelekea makumi ya maelfu ya wakimbizi kuvuka mipaka ya Sudan, na kutishia kuzusha taharuki zaidi katika eneo tete la Afrika la ukanda wa Sahel barani Afrika.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) linakadiria kuwa watu 860,000 wamehama Sudan baada ya vita kuanza.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Nairobi siku ya Jumatano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alikiri kushindwa kuzuia mapigano nchini Sudan.
Guterres alisema: "Umoja wa Mataifa ulishangazwa" na mzozo huo, kwa sababu shirika hilo la dunia na taasisi nyingine zilikuwa na matumaini kwamba mazungumzo ya kutatua mzozo wa kisiasa huko Sudan yangefanikiwa.