Ebrahim Raisi: Iran daima iko pamoja na taifa na serikali ya Syria
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye siku za Jumatano na Alkhamisi tarehe 4 na 5 Mei alikuwa kwenye ziara ya kikazi nchini Syria ameliambia shirika la habari la nchi hiyo SANA na kanali ya televisheni ya "al Suriyyah" kwamba, Iran daima imekuwa na itaendelea kuwa pamoja na taifa na serikali ya Syria katika hali zote.
Katika mahojiano hayo, Sayyid Ebrahim Raisi amesema, kama ilivyokuwa huko nyuma, hivi sasa na katika siku za usoni pia, Iran itaendelea kuwa pamoja wananchi na serikali ya Syria na itaendelea kuwemo vilivyo ndani ya kambi ya muqawama. Amesema pamoja na kuweko vitisho na vikwazo vya kila namna lakini Syria inaendelea kusimama kidete katika kupambana na kambi ya kimataifa ya shari kwa ajili ya kusimamisha amani, haki na uadilifu.
Vile vile amesema, Wamarekani wamevamia na kuyakalia kwa mabavu baadhi ya maeneo ya Syria na hivi sasa wanaendelea kupora utajiri wa nchi hiyo. Suala ambalo walishindwa kulipata kupitia magenge yao ya kigaidi, wameamua kulitekeleza kwa njia ya kuivamia moja kwa moja na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Syria. Lakini muqawama wa wananchi wa Syria utafelisha njama zote za mabeberu, Wamarekani watafukuzwa nchini humo na taifa la Syria mwishowe ndilo litakalokuwa mshindi.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha pia kuwa, njia sahihi ya kutatua daghadagha za nchi zinazopakana na Syria, ni kurejeshwa kila shibri ya ardhi ya nchi hiyo mikononi mwa serikali ya Damascus na kwamba askari yeyote wa kigeni hapaswi kuendelea kuwepo ndani ya ardhi ya Syria kinyume cha sheria.
Aidha amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Syria zina ushirikiano wa kimkakati na kwamba uungaji mkono wa Tehran kwa serikali halali ya Syria katika kipindi chote cha mgogoro; na kuisaidia serikali hiyo kupambana na magenge ya kigaidi ni ushahidi wa ushirikiano imara wa kimkakati uliopo baina ya mataifa haya mawili.