Baqeri: Mlingano wa nguvu unahama kutoka Magharibi na unaelekea Mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i97132-baqeri_mlingano_wa_nguvu_unahama_kutoka_magharibi_na_unaelekea_mashariki
Mkuu wa Majeshi ya Iran amesema kwamba, kuna kila dalili na ushahidi unaoonesha kuwa nguvu za Marekani na washirika wake wa Magharibi zinazidi kufifia na mlingano wa nguvu duniani hivi sasa umo katika kuhama kutoka Magharibi kuelekea Mashariki mwa dunia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2023 07:22 UTC
  • Baqeri: Mlingano wa nguvu unahama kutoka Magharibi na unaelekea Mashariki

Mkuu wa Majeshi ya Iran amesema kwamba, kuna kila dalili na ushahidi unaoonesha kuwa nguvu za Marekani na washirika wake wa Magharibi zinazidi kufifia na mlingano wa nguvu duniani hivi sasa umo katika kuhama kutoka Magharibi kuelekea Mashariki mwa dunia.

Meja Jenerali Mohammad Hossein Baqeri amesema hayo wakati alipoonana na kuzungumza na mkuu mwenzake wa majeshi ya Oman, Luteni Jenerali Abdullah bin Khamis al-Raisi katika mji mkuu wa Oman, Muscat leo Jumatatu.

Baqeri amelitaja eneo la Ghuba ya Uajemi na Asia Magharibi kuwa miongoni mwa maeneo muhimu na nyeti zaidi duniani, akisema kuwa Wamarekani wamekuwa wakijaribu kuimarisha nguvu zao katika eneo hili ikiwa ni sehemu ya njama zao za kutaka kuwa na ushawishi katika masuala ya kimataifa na kieneo.

Meja Jenerali Bazeri pia amesema, Tehran inajiandaa kuitisha mkutano mkubwa kuhusu mpangilio mpya wa dunia utakaohudhuriwa na nchi kadhaa ikiwemo Oman.

Amepongeza uhusiano wa kijadi, kidugu, kirafiki na wa karibu kati ya Iran na Oman na kusisitizia haja ya kuwepo ushirikiano thabiti wa kiusalama kwenye mpaka wa pamoja wa baharini.

Aidha amepongeza ushirikiano wa kijeshi kati ya Tehran na Muscat, na kuikaribisha nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi kushiriki katika mazoezi ya kijeshi yanayofanywa na majeshi ya majini ya Iran.

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Oman amesisitiza kuwa, umoja na mshikamano kati ya mataifa ya eneo hili ndiyo mambo yanayoweza kudhamini usalama katika eneo lote.

Iran na Oman zimeshafanya mazoezi kadhaa ya pamoja ya wanajeshi wa majini katika miaka ya hivi karibuni.