Nchi za Ulaya zitadidimia kwa kufuata kibubusa nyayo za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i97230-nchi_za_ulaya_zitadidimia_kwa_kufuata_kibubusa_nyayo_za_marekani
Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran anasema nchi za Ulaya zitatumbukia katika hali mbaya isiyoweza kurekebishwa ikiwa hazitafanikiwa kutupilia mbali minyororo ya kujidhalilisha mbele ya Marekani na kuunga mkono kibubusa sera za Washington.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 11, 2023 03:08 UTC
  • Nchi za Ulaya zitadidimia kwa kufuata kibubusa nyayo za Marekani

Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran anasema nchi za Ulaya zitatumbukia katika hali mbaya isiyoweza kurekebishwa ikiwa hazitafanikiwa kutupilia mbali minyororo ya kujidhalilisha mbele ya Marekani na kuunga mkono kibubusa sera za Washington.

Meja Jenerali Mohammad Hossein Baqeri aliyasema hayo Jumatano alipokuwa akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa kongamano la kimataifa la “Jiometri ya Mfumo Mpya wa Dunia” mjini Tehran.

"Mabadiliko yamekuwa kanuni inayotawala utaratibu wa ulimwengu mzima katika zama tofauti za kihistoria, na kuendelea kwa mfumo fulani hakumaanishi usahihi wake," amesema, akiongeza kuwa kambi za Mashariki na Magharibi tangu mwanzoni mwa karne ya 20 zimetaka kujifaidisha, kutawala eneo la Asia Magharibi na kutumia uwezo wake wa kimkakati."

Zaidi ya hayo, Jenerali Baqeri amesema Vita Baridi vilivyodumu kwa muda wa miaka 40, kutengwa  ukomunisti katika milinganyo ya kimataifa, uvamizi wa kikatili wa Marekani dhidi ya Afghanistan na Iraq na kuundwa kwa kundi la kigaidi la Daesh kwa nia ya kuzipindua serikali za Iraq na Syria zote zinaashiria ukweli kwamba utaratibu wa dunia unabadilika.”

Amesema kwamba kuna "ishara kwamba mfumo wa sasa wa ulimwengu wote haujapata utulivu" na ulimwengu unakaribia kuingia katika zama ya mfumo mpya.

Baqeri pia amesema uanzishwaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mojawapo ya vikwazo vikuu vya utawala na satwa ya Marekani duniani, akisema kwamba ahadi za Mwenyezi Mungu pia zinaashiria kuanguka kwa mifumo ya kiistikbari na kuanzishwa mfumo wa watu wema badala yake.

Amesisitiza kuwa, utawala ghasibu wa Israel ambao wakati mmoja ulikuwa ukifikiria kudhibiti maeneo ya Waislamu kutoka Mto Nile hadi Euphrates, sasa unazidi kuporomoka na kukumbwa na misukosuko mingi tangu kushindwa kwa fedheha katika hujuma ya siku 33 dhidi ya Lebanon katika majira ya joto ya mwaka 2006.

"Taifa linalodhulumiwa la Palestina na Mhimili wa Muqawama, kwa upande mwingine uko kwenye kilele cha uwezo wake, na unasonga mbele kwenye njia ya kuikomboa Palestina," Baqeri amebainisha.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa jeshi la Iran aidha amebainisha kuwa, China imechukua nafasi ya Marekani kama nchi yenye uchumi mkubwa zaidi duniani, na nia yake ya kuwekeza katika bara la Asia na baadhi ya maeneo ya Afrika na Ulaya inaonyesha wazi kwamba jiometri mpya ya mfumo wa dunia imeanza kujitokeza.