Iran: Tunataraji kuona uhusiano wetu na Misri unafufuliwa kikamilifu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza matumaini yake kuwa uhusiiano wa Iran na Misri utafufuliwa kikamilifu kutokana na siasa za nje za serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, ofisi za kulinda maslahi ya nchi hizi mbili zinafanya kazi zao vizuri katika miji mikuu; Tehran na Cairo na wakuu wa ofisi hizo zote mbili wanafanya kazi zao kwa ngazi ya balozi. Kwa hivyo tayari kuna njia rasmi ya mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Iran na Misri.
Amir-Abdollahian amefafanua zaidi kwa kusema, bila shaka baadhi ya nchi zimefanya jitihada za kuzihimiza Misri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuboresha uhusiano baina yao.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema kuhusu kurejeshwa uhusiano kati ya Tehran na Riyadh kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia Jumanne wiki hhii ilitangaza kurejesha shughuli zake za kibalozi hapa mjini Tehran, na karibuni hivi Iran itatangaza jina la balozi wake mpya mjini Riyadh.
Amir-Abdollahian pia amesema kuhusu kuwekwa upya kamera za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kwa ajili ya shughuli za nyuklia za Iran kwamba, hiyo ni hatua nzuri na kusisitiza kwamba, Tehran inatarajia wakala huo utaachana na tabia yake ya kuachana na masuala ya kiufundi na kuingiza siasa kwenye kadhia ya nyuklia ya Iran.
Vile vile amesema, Iran inaendelea kupokea ujumbe mbalimbali kutoka kwa Wamarekani kupitia wasuluhishi na pia inawatumia ujumbe Wamarekani akisisitiza kuwa, moja ya kazi muhimu za Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ni kufuta vikwazo na kuvifanya visifanye kazi.