Iran: Nchi za Magharibi zimegeuzwa 'pepo ya usalama' kwa magenge ya kigaidi
Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Iran amesema nchi za Magharibi ni 'pepo ya usalama' kwa makundi ya kigaidi.
Tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, zaidi ya raia na maafisa elfu 17 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameuawa shahidi na kundi la kigaidi la Munafikiana (MKO) na magenge mengine ya kigaidi.
Na tokea mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani imeyaweka magenge mbalimbali ya kigaidi chini ya kivuli cha uungaji mkono wake wa kifedha, kisiasa na kipropaganda na kuunga mkono jinai za kigaidi za magenge hayo dhidi ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kazem Gharib Abadi, Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Iran, amesema katika mazungumzo na Mar Awa Royel III Kiongozi mkuu wa Kanisa la Assyrian la Mashariki kwamba watu wa Iran ni wahanga wa ugaidi; na wakati nchi za Magharibi zimegeuzwa kuwa 'pepo ya usalama' ya makundi ya kigaidi, nchi hizo zinaituhumu Iran kuwa inaunga mkono makundi ya kigaidi.
Gharibabadi ameshiria kuwepo kwa jamii za dini za waliowachache nchini Iran na akabainisha kwamba, wakati ni vigumu sana kujenga msikiti katika nchi zinazodai kutetea haki za binadamu, kulingana na takwimu za hivi karibuni, kuna takribani makanisa 400 nchini Iran ya wafuasi wa dini ya Kikristo.
Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Iran ameashiria pia vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya watu wasio na hatia wa Iran na akasema, Iran ni nchi huru inayojitawala na haijaivamia nchi yoyote wala kukanyaga haki za nchi yoyote ile, lakini Wamagharibi wametenda ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kwa kuweka vikwazo vya upande mmoja dhidi ya watu wa Iran.
Kwa upande wake, Mar Awa Royel III Kiongozi mkuu wa Kanisa la Assyrian la Mashariki amewashukuru watu wa Iran kwa ukarimu wao na akasema, dini tukufu ya Uislamu na dini ya Ukristo, zote mbili zinatilia mkazo heshima ya utu na haki za binadamu; na Wakristo Waassyrian ni sehemu ya Iran na watoto wa kweli na waaminifu kwa Iran.../