Uchumi wa Iran unatazamiwa kustawi kwa asilimia 8%
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i97642-uchumi_wa_iran_unatazamiwa_kustawi_kwa_asilimia_8
Iran imejiwekea lengo la kufikia kiwango cha wastani cha ukuaji wa uchumi cha asilimia 8 kati ya 2023 na 2028 kama sehemu ya mpango mpya wa mustakabali uliozinduliwa na serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2023 03:17 UTC
  • Uchumi wa Iran unatazamiwa kustawi kwa asilimia  8%

Iran imejiwekea lengo la kufikia kiwango cha wastani cha ukuaji wa uchumi cha asilimia 8 kati ya 2023 na 2028 kama sehemu ya mpango mpya wa mustakabali uliozinduliwa na serikali.

Katika uchambuzi uliochapishwa Jumapili na Shirika Rasmi la Habari la Iran, IRNA, "Mojawapo ya malengo makuu na vipaumbele vya kimsingi vya Mpango wa Saba wa Maendeleo ya miaka mitano ni (kufikia) maendeleo yanayoambatana na haki na wastani wa ukuaji wa uchumi wa asilimia 8." 

Mpango mpya wa dira ya uchumi wa Iran ulizinduliwa Jumamosi na Shirika la Mpango na Bajeti la Iran (PBO), zaidi ya mwaka mmoja baada ya Mpango wa Sita wa Maendeleo wa nchi hiyo kumalizika Machi 2022.

Mipango ya dira ya miaka mitano imeweka miongozo ya jumla na shabaha za ukuaji wa uchumi nchini Iran. Serikali na mabunge nchini yanatakiwa kupitisha sera na kutekeleza vitendo visivyokiuka masharti na shabaha zilizojumuishwa katika mipango ya maendeleo.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Mohammad Mokhber (kulia) akitizama mpango wa dira ya saba ya Iran uliozinduliwa Mei 20 jijini Tehran.

Ripoti ya IRNA imesema kuwa, mpango wa dira ya saba wa Iran una hatua kuu za mageuzi ya kiuchumi ambayo zaidi yamelenga katika kuimarisha shughuli za viwanda na kilimo nchini na kuongeza thamani katika sekta za huduma na teknolojia.

Aidha ripoti hiyo imebaini kuwa mpango huo pia unaweka malengo ya kupunguza mfumuko wa bei wa Iran hadi karibu asilimia 9.5 na unatoa hatua za usimamizi bora wa usambazaji wa pesa wa nchi na mapato ya sarafu ngumu.