Kiongozi Muadhamu awausia viongozi wa serikali kufuata mwenendo wa Imam Ali (as)
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya jana alikutana na kuhutubia baraza la mawaziri kabla ya dhifa ya chakula cha futari ambapo alieleza vipengee kadhaa vya hekima za Imam Ali bin Abi Twalib (as) zilizoandikwa katika kitabu cha Nahjul Balagha.
Ayatullah Khamenei ameashiria maneno ya Imam Ali (as) kuhusu jinsi ya kuamiliana na kipindi cha fitina na kusema: Imam Ali (as) anausia kwamba katika kipindi na zama za fitina ambapo huwa vigumu kwa wananchi kumaizi baina ya haki na batili, Mwislamu anapaswa kuwa na mwenendo ambao hautakuwa na faida kwa fitina.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa katika kipindi cha fitina kama ile ya (baada ya uchaguzi wa rais) mwaka 2009 hapa nchini, matamshi ya watu, kimya chao, hatua na hata aina ya mtazamo wao haupasi kuwa kwa namna ambayo itatia nguvu mrengo wa fitina.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, yumkini baadhi ya watu wasisimame waziwazi kukabiliana na fitina kutokana na mielekeo yao makhsusi lakini pia wao hawapasi kutumiwa kwa maslahi ya mrengo wa fitina.
Vilevile ameashiria kipengee kingine cha hekima za Imam Ali bin Abi Twalib katika kitabu cha Nahjul Balagha akizungumzia mtazamo wa kuona dhamana na majukumu ya viongozi kama wenzo wa kupata utajiri na nafasi maalumu na kusema: Mtazamo kama huo kwa masuulia na majukumu ambayo kwa hakika ni amana, humfanya mtu kuwa hakiri na duni.
Vilevile amezungumzia nasaha za Imam Ali bin Abi Twalib kuhusu jinsi ya kulinda ulimi na kusema: Daima tunapaswa kulinda ndimi zetu kwa sababu matatizo mengi ya mwanadamu yanatokana na ulimi.