Iran yataka kuondolewa vizuizi vinavyokwamisha kufikishwa misaada Yemen
Mshauri Mkuu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametaka kuondolewa vizuizi vyote vinavyokwamisha kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Yemen.
Ikiwa ni muendelezo wa mashauriano na juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kupigania kutatuliwa mgogoro wa Yemen, kupatikana amani ya kudumu na kupunguziwa mateso na masaibu wananchi wa nchi hiyo, Ali Asghar Khaji, mshauri mkuu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala maalumu ya kisiasa jana Jumatatu alifanya mazungumzo kwa njia ya video, na Hans Grundberg, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Yemen na kubadilishana naye maoni kuhusu njia za kuutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Matukio ya hivi karibuni ya Yemen, mchakato wa mazungumzo huko Sana'a na hatua zitakazochukuliwa baadaye katika jitihada za kusuluhisha mgogoro wa Yemen ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa na wawili hao hiyo jana Jumatatu.
Mshauri Mkuu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala Maalumu ya Kisiasa ameelezea kuridhishwa kwake na fursa zilizojitokeza hivi sasa, hususan mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Saudi Arabia na Ansarullah huko Sana'a, na kutaka kuondolewa vikwazo vilivyopo kama njia ya kuruhusu kuwafikia watu wa Yemen, misaada ya kibinadamu.
Kwa upande wake, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen amesisitizia ulazima wa kuendelea mazungumzo ya kisiasa ili kujenga imani na kufikia makubaliano kati ya pande hizo mbili, kwa ajili y aamani ya kuduumu huuko Yemen.