Iran yasambaratisha mtandao wa kijasusi unaoshirikiana na mashirika ya kijasusi ya kigeni
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imewakamata wanachama wa mtandao wa kijasusi ambao walikuwa wanajishughulisha na mradi unaoendeshwa na shirika moja la kigeni la kijasusi kupata habari kuhusu Wairani wanaosafiri nje ya nchi.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne, wizara hiyo ilisema kuwa shirika hilo la kijasusi limekuwa likiwafuatilia Wairani wenye majukumu katika nyadhifa tofauti au utaalamu maalum katika nyanja mbalimbali na vilevile wale wanaopata taarifa muhimu katika taasisi nyeti za nchi.
Wizara hiyo ilibaini kuwa hatua zake zilipelekea kutambuliwa kwa " mawakala watendaji" wa mtandao huo katika mashirika na taasisi kadhaa za Iran.
Taarifa hiyo ilisema shirika moja la kijasusi la kigeni lilimwambia mmoja wa majasusi wake majina ya walengwa wake miongoni mwa Wairani wanaosafiri nje ya nchi. Jasusi huyo alitoa majina kwa maajenti wake hadi kuwafikia waendeshaji wa mifumo ya kiidara katika mashirika kadhaa.
Waendeshaji hao wa mifumo ya kiidara walitumia hifadhidata yao na kutoa taarifa za walengwa na kuziwasilisha kwa majasusi ndani ya nchi ambao walihamisha taarifa hizo kwa kinara wa mtandao huo ambaye alizifikisha kwa shirika la ujasusi la serikali ajinabi.
Hayo yanaripotiwa wakati ambao, siku ya Jumapili, Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran ilitangaza kwamba vikosi vyake vilivamia timu ya magaidi yenye mafungamano na shirika la kijasusi la utawala haramu wa Israel Mossad katika eneo la magharibi mwa nchi.
Aidha, mapema wiki hii, vikosi vya usalama wa taifa katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) vilisambaratisha mtandao wa kigaidi wenye mafungamano na kundi la kigaidi la Daesh Khorasan (Daesh-K) katika mkoa wa kusini mwa Iran wa Fars.