Wagonjwa milioni 1.2 wa kigeni watibiwa katika hospitali za Iran
Waziri wa Afya wa Iran Bahram Einollahi anasema kuwa nchi yake imepata maendeleo makubwa katika sekta ya afya tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979, na kuongeza kuwa zaidi ya wagonjwa milioni 1.2 wa kigeni walitibiwa katika hospitali za Iran mwaka jana.
"Leo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya nchi bora zaidi katika uwanja wa afya, si tu katika eneo hili bali pia ulimwenguni," Einollahi alisema hayo jana Jumapili katika mkutano wa wawakilishi wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi.
Akiashiria utafiti wa wanafunzi 7,000 wa kigeni katika fani ya afya nchini Iran, Einollahi alisema, “Mwaka jana, tulitibu wagonjwa wa kigeni zaidi ya 1,200,000 katika hospitali za humu nchini, wengi wao wakiwa ni kutoka Afghanistan, Iraq, Azerbaijan, Pakistan, Uturuki, India, Armenia, Turkmenistan, Lebanon na Tajikistan.”
Waziri wa Afya wa Iran amegusia pia maendeleo ya utalii wa afya humu nchini na kusema, wagonjwa wengine ni wale wa magonjwa ya wanawake na uzazi, upasuaji wa macho, mifupa, magonjwa ya moyo na mishipa, mkojo, saratani, msongo wa mawazo na kadhalika ndiyo magonjwa ambayo sana huwafanya watu kutoka nje ya Iran kuja kutafuta matibabu humu nchini.
Amesema, watalii wa afya wanaamini na wanakiri kwamba madaktari wa Iran wana ujuzi na uwezo wa hali ya juu katika fani zao.
Amesema: "Gharama ya chini na ubora wa hali ya juu wa matibabu kwa kutumia teknolojia ya kisasa, mbinu mpya za matibabu, mambo ya kawaida ya kitamaduni na kihistoria, kuwafikia kiurahisi madaktari nchini Iran na vivutio vya watalii ni miongoni mwa sababu za watalii kuchagua kuja Iran kupata huduma za matibabu."
Akiashiria ulazima wa kuundwa "ukanda salama" kwa ajili ya uhamishaji wa wagonjwa wa kigeni kuja hapa Iran, Waziri Einollahi amesema, vituo 233 vya matibabu vya Iran vimepokea kibali cha kimataifa cha kupokea watalii wa kimatibabu, takwimu ambayo ina nafasi ya kutosha ya kuwa kubwa zaidi.