Kiongozi Muadhamu: Kulinda uhuru, maslahi ya taifa kunafungamana na kulindwa imani, matumaini
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kulinda uhuru na heshima na maslahi ya taifa kunafungamana na kudumisha imani na matumaini.
Akizungumza leo mbele ya hadhara kubwa ya wananchi katika kumbukumbu ya mwaka wa 34 tangu kuaga dunia Imam Ruhullah Khomeini (RA) katika Kaburi lake kwenye viunga vya mji wa Tehran, Ayatullah Ali Khamenei amemtaja Imam kuwa mmoja wa vinara wa historia ya Iran na kwamba hakuna upande wowote unaoweza kumfuta katika kumbukumbu ya historia au kupotosha sura yake kwa muda mrefu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja mageuzi matatu makubwa yaliyofanywa na Imam Khomeini (M.A) nchini, katika Umma wa Kiislamu na ulimwenguni kwa ujumla na kubainisha kuwa: "Imani na matumaini ya Imam vilikuwa programu laini (software) na chanzo cha kudhihiri mageuzi haya makubwa ya kihistoria, na kila harakati na mrengo unaotaka kulinda maslahi ya taifa, hali bora ya kiuchumi, maendeleo na hadhi ya taifa la Iran unapasa kufanya juhudi za kuimarisha imani na matumaini ya wananchi na jamii nzima kwa ujumla.
Akizungumzia mageuzi yaliyofanywa na Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei ameashiria mwamko wa Kiislamu, harakati na utayarifu wa Umma wa Kiislamu na kulifanya suala la Palestina kuwa kadhia ya kwanza ya Ulimwengu wa Kiislamu na kusema: Imam alitia uhai katika mwili uliokuwa umedhoofika wa taifa la Palestina na hivi sasa Siku ya Kimataifa ya Quds imekuwa jukwaa la kuwaunga mkono raia wa Palestina wanaodhulumiwa si tu nchini Iran bali pia katika miji mikuu ya nchi zisizo za Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema mahitaji na suhula za lazima zinazohitajika kwa ajili ya kufuata njia na malengo ya Imam Khomeini vinatofautiana na mbinu za miaka 40 iliyopita na kuongeza kuwa: Bila shaka safu za maadui hazijabadilika; na leo hii kama ilivyokuwa jana, harakati ya ubeberu, kambi ya wazayuni na ile ya madhaimu wachokozi zimesimama katika safu moja dhidi ya taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Katika miongo kadhaa iliyopita, taasisi fedhuli za ubeberu na vyombo vyao vya kiusalama, kisiasa na kifedha vilifanya kila linalowezekana ili kudhoofisha imani na matumaini ya wananchi ambapo walifanikiwa katika baadhi ya mambo; hata hivyo katika kadhia nyingi walishindwa na kufeli mbele ya wananchi wa Iran.
Ameyataja machafuko na ghasia za karibuni hapa nchini kuwa ni katika njama hizo za maadui. Amesema: Ghasia hizo zilipangwa na taasisi za nchi za Magharibi na kutekelezwa kwa msaada mkubwa wa kifedha, silaha na vyombo vya habari vya mashirika ya usalama ya Magharibi na mamluki na vibaraka wao wanaoendesha sera za uhasama dhidi ya Iran.