Rais wa Iran: Huduma za Mapinduzi ya Kiislamu zielezwe kwenye majukwaa mbalimbali
-
Rais Ebrahim Raisi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kuna udharura wa wananchi hususan kizazi cha vijana kuelezwa mageuzi makubwa yaliyosababishwa na Harakati ya tarehe 15 Khordad, na ametoa wito wa kubainishwa huduma na hatua zinazochukuliwa na Mapinduzi ya Kiislamu katika majukwaa mbalimbali.
Rais Ebrahim Raisi ameyasema hayo leo Jumatatu inayosadifiana na tarehe 15 Khordad 1402 Hijria Shamsia, siku ya kumbukumbu ya harakati ya kihistoria ya Imam Khomeini (RA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mwaka 1342 Hijria (1963 Miladia).
Harakati hiyo ya tarehe 15 Khordad 1342 (Juni 1963) ilikuwa nukta kuu ya mageuzi makubwa katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu na mwanzo wa harakati ya Kiislamu ya taifa la Iran.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran (IRNA), Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi amesema katika kikao na wajumbe wa Kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya mwaka wa 60 wa harakati ya kihistoria ya Khordad 15 kuwa, moja ya majukumu muhimu ya kongamano hilo ni kukumbusha dhulma na ukatili wa utawala wa kifalme wa Pahlavi na pia kueleza huduma na mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa wananchi.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja msukumo wa wananchi katika harakati ya kihistoria la Khordad 15 kuwa ni matumaini ya kufanya mabadiliko kwa manufaa ya Uislamu na wananchi wa Iran na kuongeza: Siku hiyo wakati watu wa Varamin, Kusini Mashariki mwa Tehran, walipoanza harakati yao, waliwajihiana na utawala uliokuwa umejizatiti kwa silaha wa Pahlavi, lakini walikuwa tayari kufa shahidi katika njia hiyo kwa matumaini ya kufanya mabadiliko.
Tarehe 15 Khordad miaka 60 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran baada ya kupata habari kwamba Imam Ruhullah Khomeini (MA) alikuwa amekamatwa na utawala dhalimu wa Shah, walifanya maandamano makubwa kote nchini dhidi ya utawala huo.
Siku kadhaa kabla yake, Imam Khomeini alikuwa ametoa hotuba kali katika Chuo cha Kidini cha Faidhiyya akifichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah, jambo ambalo liliuchukiza sana utawala huo na kuamua kumtia nguvuni. Suala hilo liliwakasirisha sana wananchi wa Iran ambao waliamua kufanya maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwake mara moja.
Harakati hiyo ya mapambano ilikuwa mwanzo wa mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi shupavu wa Iran dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Shah, mapambano ambayo yaliainisha mustakbali wa kisiasa na kijamii wa Iran.
Mapambano hayo yaliendelea kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi mwaka 1979.