Ubalozi wa Iran nchini Saudi Arabia wafunguliwa tena
Ubalozi wa Iran nchini Saudi Arabia umefunguliwa tena ikiwa ni miezi mitatu baada ya makubaliano ya kurejeshwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, ubalozi wa Iran ulifunguliwa rasmi tena jana Jumanne mjini Riyadh, ikiwa ni miezi mitatu baada ya makubaliano ya kurejesha uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia.
Juzi Jumatatu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitangaza kuwa Ubalozi wa Iran mjini Riyadh utafunguliwa rasmi siku ya Jumanne.
Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema: Ubalozi wa Iran mjini Riyadh, ubalozi mdogo wa Iran mjini Jeddah na ofisi ya mwakilishi wa kudumu wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu vitafunguliwa rasmi siku za Jumanne na Jumatano.
Mwezi Aprili mwaka jana, Iran ilimteua Alireza Enayati, mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Iran, kuwa balozi wa Iran nchini Saudi Arabia. Katika mwezi huo huo, wajumbe kutoka Iran walitembelea Saudia kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kufungua tena ubalozi wa Iran mjini Riyadh na balozi zake za kidiplomasia nchini humo.
Muda mfupi kabla ya hapo, wajumbe kutoka Saudi Arabia walikuwa wamekuja hapa Tehran kuchunguza namna ya kufunguliwa tena ubalozi wa Saudia na ubalozi wake mdogo humu nchini Iran.