Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Brunei Darussalam zasisitiza kuimarisha ushirikiano
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Brunei wamekutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na kusisitiza udharura wa kukuza zaidi ushirikiano baina ya mataifa yao.
Akiongoza ujumbe wa ngazi za juu, Dato Erywan Pehin Yusof, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Brunei Darussalam amefanya ziara mjini Tehran kwa mwaliko wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Hussein Amir-Abdollahian.
Jana, ujumbe wa Brunei ulifanya mkutano na mwanadiplomasia mkuu wa Iran na maafisa kadhaa wa wizara ya mambo ya nje ya Iran.
Ajenda kuu za mazungumzo hayo zilikuwa ni kuendeleza maingiliano na ushirikiano kati ya Iran na Brunei na kuyaangalia kwa kina zaidi masuala muhimu zaidi ya kieneo na kimataifa.
Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili walikutana na kujadiliana kando ya kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York mwaka jana.
Hossein Amir- Abdollahian alisema katika mkutano na mwenzake wa Brunei mjini New York kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kuendelezwa uhusiano wa pande mbili na Brunei.
Katika kikao hicho Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Brunei alikaribisha kuongezwa ushirikiano katika ngazi mbalimbali na Iran na kueleza matumaini ya kuongezeka mikutano na mabadilishano ya wajumbe na kusisitiza kuwa, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili utaendelea katika vikao vya kimataifa.