Jeshi la IRGC ya Iran lavunja mtandao wa magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i98784-jeshi_la_irgc_ya_iran_lavunja_mtandao_wa_magaidi
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limefanikiwa kusambaratisha mtandao wa magaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, kusini mashariki mwa Iran.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Jun 14, 2023 23:20 UTC
  • Jeshi la IRGC ya Iran lavunja mtandao wa magaidi

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limefanikiwa kusambaratisha mtandao wa magaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, kusini mashariki mwa Iran.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na SEPAH imeeleza kuwa, vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu vimewaangamiza magaidi wawili, mbali na kumtia mbaroni mmoja kwenye operesheni hiyo.

Maafisa wa SEPAH wamefanikiwa pia kukamata idadi kubwa ya silaha na mada za miripuko zilizoingizwa nchini kimagendo na magaidi hao. IRGC imesema baadhi ya silaha zilizokamatwa katika operesheni hiyo ni pamoja na bunduki za aina kadhaa ikiwemo ya AK-47, maguruneti, mada za miripuko na risasi.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran iliwakamata wanachama wa mtandao wa kijasusi ambao walikuwa wanajishughulisha na mradi unaoendeshwa na shirika moja la kigeni la kijasusi kupata habari kuhusu Wairani wanaosafiri nje ya nchi.

Askari wa SEPAH

Kabla ya hapo, Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran ilitangaza kwamba vikosi vyake vilivamia timu ya magaidi yenye mafungamano na shirika la kijasusi la utawala haramu wa Israel Mossad katika eneo la magharibi mwa nchi.

Aidha, vikosi vya usalama wa taifa katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) hivi karibuni vilisambaratisha mtandao wa kigaidi wenye mafungamano na kundi la kigaidi la Daesh Khorasan (Daesh-K) katika mkoa wa kusini mwa Iran wa Fars.