Iran na Kenya zatiliana saini hati tano za ushirikiano
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99818-iran_na_kenya_zatiliana_saini_hati_tano_za_ushirikiano
Iran na Kenya zimetiliana saini hati tano za ushirikiano katika nyuga tofauti za mawasiliano, uvuvi, kilimo, afya na elimu ya ufundi, maarifa na matibabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 12, 2023 03:54 UTC
  • Iran na Kenya zatiliana saini hati tano za ushirikiano

Iran na Kenya zimetiliana saini hati tano za ushirikiano katika nyuga tofauti za mawasiliano, uvuvi, kilimo, afya na elimu ya ufundi, maarifa na matibabu.

Kwa mujibu wa IRNA, hati za ushirikiano baina ya Iran na Kenya zimetiwa saini leo mbele ya Rais Ebrahim Raisi na mwenyeji wake Rais William Samoei Ruto jijini Nairobi.

Rais wa Iran amewasili mjini Nairobi alfajiri ya leo kikiwa ni kituo cha kwanza cha safari yake ya kuzitembelea nchi tatu za Afrika za Kenya, Uganda na Zimbabwe.

Muda mchache baada ya kuwasili, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Rais amepokewa rasmi na mwenyeji wake, Rais William Ruto wa Kenya katika Ikulu ya Nairobi na amepigiwa mizinga 21 kwa heshima yake.

Marais wa Iran na Kenya wakipeana mikono baada ya kuzungumza na waandishi wa habari jijini Nairobi leo Jumatano, Julai 12, 2023

 

Mara baada ya hafla ya kukaribishwa rasmi, marais wa Iran na Kenya wameanza mazungumzo ya faragha na baadaye kumetiwa saini hati tano muhimu za ushirikiano wa pande mbili kati ya Iran na Kenya mbele ya marais hao wawili. Hati hizo zinahusiana na sekta za mawasiliano, uvuvi, kilimo, afya na elimu ya ufundi, maarifa na matibabu.

Katika ziara yake hiyo, Rais Ebrahim Raisi anaongoza ujumbe wa ngazi za juu wa Iran akiwemo Waziri wa Afya, Waziri wa Jihadi ya Kilimo, Waziri wa Mambo ya Nje na maafisa wengine wa ngazi za juu wa sayansi na teknolojia wa Jamhuri ya Kiislamu. 

Jana usiku na kabla ya kuanza safari ya kuelekea Nairobi Kenya, Rais Raisi alisema katika Uwanja wa Ndege wa Mehrabad hapa Tehran kwamba lengo la safari yake ya kuzitembelea nchi hizo tatu za Kenya, Uganda na Zimbabwe ni kuitikia mwaliko rasmi wa marais wa nchi hizo na kuimarisha ushirikiano na nchi hizo akisisitiza kuwa bara la Afrika linapewa umuhimu mkubwa na siasa za mambo ya nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.